Viongozi wa Umoja wa UIaya watayajadili masharti ya
mageuzi yanayopendekezwa na Uingereza na suala la mgogoro wa wakimbizi katika
mkutano wa kilele unaoandaliwa leo mjini Brussels.
Changamoto hizo mbili zinatishia umoja wa jumuiya
hiyo mnamo mwaka huu unaomalizika ambao umekuwa mojawapo ya vipindi vigumu
kabisa katika historia yake.
Viongozi 28 wa Umoja wa UIaya kwanza wataujadili
mpango wenye utata wa jeshi jipya la Umoja wa UIaya ambalo huenda likaweka doria
katika mipaka bila idhini ya nchi mwenyeji, ili kudhibiti uhamiaji wakiwemo
wakimbizi wanaotoka katika maeneo ya vita kama vile Syria.
Wakati wa chakula cha jioni mjini Brussels, Waziri
Mkuu wa Uingereza David Cameron kisha atawasilisha masharti yake kwa mara ya
kwanza kwa wenzake, akilenga kupata muafaka katika mkutano ujao wa kilele mwezi
Februari ili kuepusha Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya kitu
kinachofahamika maarufu kama “Brexit”.
Lakini mjadala huo unatarajiwa kuwa wa kishindo kwa
sababu viongozi wengine 27 wa umoja huo inaaminika kuwa wanapinga kwa kauli
moja sharti kuu la Uingereza ambalo ni kusubiri kwa miaka minne kabla ya
wahamiaji wa Umoja wa Ulaya wanaofanya kazi Uingereza kuweza kupewa mafao yao.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kiongozi mwenye
nguvu kubwa barani Ulaya, alionya katika mkesha wa mkutano huo wa kilele kuwa
suala la ujumuisho katika Umoja wa Ulaya halipaswi kujadiliwa, huku rais wa
umoja huo Donald Tusk akisema “hakuna miiko” kuhusu suala hilo.
Mkutano huo wa kilele unahitimisha mwaka uliokuwa
mgumu sana kwa Umoja wa Ulaya ambao umeufanya umoja huo kupambana na mkururo wa
migogoro; – Ukraine, Ugiriki, uhamiaji, mashambulizi ya Paris na masharti ya
Uingereza – ambayo yanatishia ndoto ya baada ya vita kuu ya dunia ya kuwa na
bara lililoungana.
Mara nyingi, tatizo kuu limekuwa lile lile – fikra
za kifedha na umoja wa kijiografia bila muundo wa kisiasa wa kuziunga mkono
fikra hizo.
Wakati kukiwa na kuongezeka kwa vuguvugu la siasa za
kizalendo na hofu kuwa mkataba wa Schengen wa Umoja wa UIaya unaoruhusu watu
kutembea kwa uhuru kati ya nchi wanachama huenda ukavunjika, Umoja wa Ulaya
uliogawika umeandaa msururu wa mikutano ya kilele ya dharura kuhusu mgogoro huo
mwaka huu ili kutafuta ufumbuzi.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameiomba jumuiya hiyo
kuweka ulinzi katika mipaka yake, kwa sababu ya mgogoro wa wahamiaji na pia kwa
sababu za kiusalama hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Novemba mjini
Paris.
Lakini mpango huo wa mpakani uliozinduliwa Jumatano,
huenda ukasababisha mvutano katika mkutano wa leo wa kilele, huku Poland
ikiutaja kuwa wa “kushangaza”.
Viongozi wanane wa Umoja wa UIaya kutoka kile
kinachoitwa “muungano wa walio na nia” unaoogonzwa na Merkel wataandaa mkutano
mdogo wa kilele na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu kabla ya mkutano mkuu
ili kujadili mpango wa kuwapa hifadhi wakimbizi moja kwa moja kutoka Uturuki.
0 comments:
Post a Comment