Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco),
Felchesmi Mramba, amewasimamisha kazi maofisa 10 wakiwamo wahasibu waandamizi
na mafundi kwa kusababisha upotevu wa mapato zaidi ya Sh.milioni 100.
Hasara hiyo ilitokea katika mfumo wa mita kupitia minara
ya simu za mkononi na faini Sh. milioni 198.1 za wateja waliobainika kuiba
umeme kwa kuchakachua mita zao.
Hata hivyo, shirika hilo limefanikiwa kuokoa fedha hizo
zilizotokana na umeme wenye thamani ya Sh. 100,248,386.42 uliotumika bila
kulipiwa pamoja na faini kutoka kwa wateja waliojihusisha na wizi wa umeme
Sh.
198,105,928.68. Kadhalika, shirika baada ya kufanya msako
mkali limefanikiwa kukamata taasisi binafsi na za serikali pamoja na watu
binafsi wakijihusisha na kuhujumu shirika hilo,ikiwemo Shule ya Sekondari ya
Jangwani (Sh. 11,023,238.00), Diwani wa Kata ya Sinza C, Joseph Marandu (Sh.
3,443,555.00), Royal Oven Bakery Kawe, (Sh. 4,112,614.00), Havan Hotel, Mbezi
Beach (Sh.1,847,913.00) na Kampuni ya Simu ya Viettel Mtwara (Sh. 524,554.76).
Wengine ni, Kampuni ya Saffa Petroleum ya Mkoani
Pwani (Sh. 16,105,235.00), Msanii wa Filamu Nchini, Wema Sepetu (Sh.
8,200,496.20) na Kampuni ya Leadcom (Sh. 13,694,632.81).
“Zoezi hili ni endelevu kwa nchi nzima na
tutaendelea kuwakamata, kuwatangaza na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria
wale watakaobainikiwa kulihujumu shirika hatutaogopa wadhifa wala umaarufu wa mtu
ama taasisi” alisema Mramba katika mkutano wake na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam.
Alisema mapema Desemba 6, mwaka huu alitoa taarifa
kwa wale wote wanaojihusisha na wizi wa umeme ama wenye mita zenye matatizo,
lakini walijisalimisha ni watu 30 na kati ya watu 2,156 waliokaguliwa 138
walikutwa na dosari mbalimbali katika mita zao na walilipishwa faini.
Akifafanua, alisema fedha zinazotakiwa kulipwa ni Sh.
milioni 198.1 na zilizokwishalipwa ni Sh. milioni 44.9 wakati waliofikishwa
kwenye vyombo vya sheria ni watu 37 kwa makosa mbalimbali. Akizungumzia kuhusu
hatua atakazowachukulia watumishi 10 aliowasimamisha kazi, Mramba alisema
uchunguzi unaendelea na fedha wanazodaiwa kuzifanyia udanganyifu zitalipwa na
kampuni ya simu husika.
Mramba alisema ili kuhakikisha kero za huduma
zinamalizika, katika kila ofisi ya kitengo cha dharula kutakuwa na Ofisa
wa huduma kwa wateja na mhandisi ambao watasimamia muda na ubora wa huduma
wanazopata wateja baada ya kutoa taarida za dharura. “Kuanzia sasa kazi
ya mafundi inapokamilika maofisa hawa niliowataja watawajibika kuwapigia simu
wateja waliotoa taarifa kuhakiki kama kazi zimefanywa kwa wakati na mteja
ameridhika … utaratibu huu utaanza leo (jana),” alisema Mramba.
0 comments:
Post a Comment