Image
Image

Kamati za Bunge zafumuliwa, wabunge wa CCM wateta.

KAMATI za Bunge zimefanyiwa mabadiliko, ikiwemo kuunda mpya mbili, kubadilishwa majina na nyingine kuunganishwa na kuwa moja.
Hatua hiyo imefikiwa kwa ajili ya kuendana na mabadiliko ya muundo wa wizara katika Serikali ya Awamu ya Tano, alizounda Rais John Magufuli.
Wakati hayo yakifanyika, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana walianza semina elekezi mjini Dodoma chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana kwa kile kilichodelezwa ni kujipanga kufanya kazi za Bunge.
Akizungumzia mabadiliko kwenye kamati za Bunge, Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, alitaja kamati mpya zilizoundwa ni Kamati ya Sheria Ndogo na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Serikali.
Akizungumza na gazeti hili, Mwandumbya alisema mabadiliko hayo ya muundo wa kamati, yameshapitishwa na Kamati ya Kanuni ya Bunge, iliyoundwa rasmi wiki iliyopita na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kwa upande wa zilizounganishwa, ni Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na kuunda kamati moja ambayo ni Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Pia kamati mbili ambazo awali zilikuwa ni Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, pia zimeunganishwa na kuwa kamati moja ambayo ni Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Pia kupitia mabadiliko hayo, kamati zilizofanyiwa marekebisho katika majina yake ni Kamati ya Viwanda na Biashara ambayo sasa inakuwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira pia imebadilishwa na sasa inakuwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Aidha, Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa sasa imebadilika na kuwa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Mwandumbya alitaja kamati ambazo hazikubadilishwa ni Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge; Masuala ya Ukimwi; Katiba, Sheria na Utawala; Kilimo, Mifugo na Maji; Miundombinu; Hesabu za Serikali; Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya Nishati na Madini.
Alisema keshokutwa Spika Ndugai anatarajiwa kutangaza majina ya wabunge, kulingana na alivyowapangia majukumu kwenye kamati hizo kabla ya kamati hizo kuanza kazi rasmi.
“Kazi ya kwanza ya kamati hizi itakuwa ni kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati, na baada ya uchaguzi huo, kamati zote zitaandaa mpangokazi hadi Januari 23, mwaka huu,” alisisitiza.
Mkutano wa pili wa Bunge la 11 unatarajiwa kuanza rasmi Januari 26, mwaka huu na utakuwa ni wa wiki mbili. Wabunge CCM wajipanga Wakati huo huo, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika semina elekezi chini ya Katibu Mkuu, Kinana, walielekezwa kwamba kikao hicho kitakuwa cha mashauriano ya namna watakavyojipanga kufanya kazi za Bunge wakiwa wana CCM.
Nje ya ukumbi wa mkutano wabunge hao, wakiwemo mawaziri, walifika na kutakiwa kusaini fomu maalumu kabla ya kuingia kwenye chumba cha mkutano.
Kinana alifungua mkutano huo akisema, “Kwa kweli kikao hiki ni cha mashauriano zaidi ya namna tutakavyojipanga kufanya kazi za Ubunge kazi za CCM ndani ya Bunge, ninyi ni mashahidi serikali kuu imeshaundwa, serikali za mitaa zimeundwa kwa maana ya halmashauri za mitaa zimekamilika.” “Sasa tunaenda kuanza kikao cha kwanza cha kazi cha Bunge. Nyinyi wabunge wa CCM ni wabunge wenye serikali,” alisema Kinana.
Kikao hicho ambacho kilianza saa 3:30, kinaelezwa kuwa ni cha siku mbili
.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment