Image
Image

Mayanja asema ana kazi kubwa ya kufanya kubadili mfumo wa uchezaji wa timu ya Simba.

KOCHA wa muda wa Simba, Jackson Mayanja amesema bado ana kazi kubwa ya kufanya kubadili mfumo wa uchezaji wa timu hiyo ili kuleta burudani kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo.
Mayanja aliyechukua mikoba ya Dylan Kerr aliyefutwa kazi wiki iliyopita, ameanza vyema kibarua chake kwa kuiongoza Simba kushinda bao 1-0, dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa 14, uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam juzi.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa pambano hilo Mayanja, alisema amefurahi kuanza vizuri kibarua chake lakini bado ana kazi ya kufanya kuhakikisha timu hiyo inaonesha kiwango cha kuvutia na ushindi kwa sababu ni timu kubwa Tanzania.
“Tumefanya mazoezi kwa siku tatu kabla ya mchezo wa leo (juzi), lakini nimefurahi kuona mabadiliko kidogo tofauti na ilivyokuwa mwanzo, lakini bado sijaridhika nataka kuongeza wingi wa mazoezi ili kuwaweka fiti wachezaji wangu ili siyo tu tupate ushindi, lakini pia tuoneshe kiwango cha kuvutia kwa sababu Simba ni timu kubwa Tanzania,” alisema Mayanja.
Kocha huyo raia wa Uganda alisema kazi ya kuwaweka fiti wachezaji wake amepanga kuifanya taratibu ili asiwachanganye na kofia kuwachosha wakashindwa kutimiza majukumu yao katika mechi za Ligi Kuu.
Kwa upande wake kocha wa Mtibwa Sugar Mecky Maxime, aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonesha kiwango kizuri ingawa hawakuweza kusawazisha bao hilo la mapema lililofungwa dakika ya sita na Hamisi Kiiza.
Maxime, alisema uchovu ndiyo kitu kikubwa kilichosababisha kupoteza mchezo huo lakini kitu pekee anachojivunia ni kwamba timu yake haikupoteza shepu ya uchezaji, licha ya uchovu waliokuwa nao uliotokana na fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA ya Uganda wiki iliyopita.
Maxime alisema licha ya kupoteza mchezo huo, bado lengo lao lipo palepale kuhakikisha msimu huu wanapambana kupigania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kama ilivyokuwa msimu wa mwaka 1999 na 2000.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment