Image
Image

Tujitahidi kuwekeza katika lishe kwa maendeleo yetu.

TOFAUTI na watu wengi wanavyofikiria kuwa lishe ni kula na kushiba, tafsiri sahihi ya lishe bora ni hali ya mwili kupokea chakula chenye virutubisho vyote muhimu kwa ajili ya kuujenga, kuukinga na kuupa joto ili kuuwezesha kufanya kazi vizuri.
Katika semina iliyoendeshwa na Jukwa la Lishe Tanzania (PANITA) kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari mjini Morogoro mwishoni mwa wiki, iligundulika kwamba mtu anaweza akala kila siku na kushiba, lakini akawa hapati kile ambacho mwili wake unahitaji na hivyo akawa na tatizo la lishe, na kuwa rahisi kuandamwa na magonjwa.
Kwa wengi, imekuwa ikichukuliwa kwamba utapiamlo ni mwili kupungukiwa na protini na wanga, lakini ukweli ni kwamba ni pamoja na kupungukiwa vitamini muhimu mwilini na madini. Siku hizi utapiamlo unachukuliwa pia kama hali ya kula chakula kingi kuliko mwili, unavyohitaji na hivyo mtu kuwa na uzito uliozidi.
Magonjwa kama upungufu wa damu, goita, kushindwa kuona vizuri na kuzaa watoto wenye migongo wazi na vichwa vikubwa ni matokeo ya upungufu (utapiamlo) wa madini kama ya joto na baadhi ya vitamini.
Hata hivyo, tatizo kubwa liko kwa watoto wanaopata upungufu wa vitamini, madini na virutubisho vyote muhimu ndani ya siku 1,000 tangu mimba zao zitungwe. Hao hupata udumavu, ambayo ni hali ya akili zao kutokua hadi kufikia kiwango kinachotakiwa.
Madhara ya hali hiyo ni watoto kuwa rahisi kuambukizwa maradhi, uwezo wao wa darasani kuwa hafifu na hata wakishakuwa watu wazima, wanakuwa na uwezo hafifu wa kufanya maamuzi ya busara.
Katika muktadha huo, familia na hata serikali hulazimika kuwatibu watu wanaougua mara kwa mara kutokana na miili yao kutohimili magonjwa, familia pia hushindwa kuzalisha kutokana na muda mwingi kumhudumia mgonjwa. Halikadhalika, mtu mwenye utapiamlo, hawezi kuzalisha ipasavyo kulinganisha na mweye lishe bora.
Takwimu zinaonesha kwamba Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na watoto weye udumavu Afrika, ikiwa nyuma ya Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 42 ya watoto nchini umri wa miaka mitano, wanakabiliwa na udumavu nchini, kiwango ambacho PANITA wanasema ni kikubwa sana. Ili kuondokana na hali hii inashauriwa kuwekeza katika lishe, kuanzia ngazi ya familia hadi serikali yenyewe.
Taarifa ya kimataifa kuhusu hali ya lishe duniani ya mwaka jana 2015, inaonesha kwamba unapowekeza Sh 2,183, tarajia kupata Sh 34,928 kutokana na uwekezaji huo.
Takwimu zinaonesha pia kwamba kama elimu ya lishe itasambaa, gharama za chakula kwa ajili ya kujenga afya bora ya mtu, hususan watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, si kubwa na vyakula hitajika vinapatikana kila mahala. Yaani si lazima uwe tajiri kula lishe bora.
Inakadiriwa kwamba haizidi Sh 600 kwa siku kwa ajili ya kumlisha mtoto mmoja lishe bora. Wataalamu wanasema yai moja la kuku wa kienyeji mara moja kwa wiki, kikombe kimoja cha maziwa na kula matunda na mboga za majani mara kwa mara, inatosha kuboresha afya zetu. Hivyo, hatuna budi tuwekeze katika lishe kwa maendeleo yetu.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment