Image
Image

Rais Magufuli aanika uozo wa Mfanyakazi wa TRA anayelipwa mishahara yawatu 17.

RAIS Dk. John Magufuli, ameanika madudu aliyoyakuta ndani ya Serikali ikiwemo mmoja wa mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kulipwa mishahara ya watu 17 na kuagiza mfanyakazi huyo afikishwe mahakamani.
Pamoja na hali hiyo amesema wapo watumishi wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi Sh milioni 40 kwa mwezi ambayo sasa  itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi Sh milioni 15.
Rais Magufuli alitoa taarifa hiyo jana nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo alihutubia kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais.
Dk. Magufuli alisema Serikali yake imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo.
“Kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa shilingi bilioni 1 na milioni 800 na kwamba ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima utaisaidia Serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za Watanzania.
“ Leo (jana) hii yupo mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato TRA ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17 na huyo ni lazima afikishwe mahakamani.
“…serikali imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo, lakini kwa wale wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi shilingi milioni 40, itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi shilingi milioni 15,” alisema Rais Magufuli.
Alisema anashangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuishi kama malaika huku wengine wakiishi kama masheteni, jambo ambalo halina nafasi katika Serikali yake.
“Nyiye mliokuwa mnaishi kama malaika, sasa zamu yenu kuishi kama mashetani,” alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.
Misaada ya wafadhili
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli, amewataka Watanzania kuchapa kazi kwa juhudi ili nchi iondokane na utegemezi wa misaada ya wafadhili ambayo huandamana na masharti.
Alisema jukumu kubwa lililo mbele kwa sasa ni kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja ahakikishe anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.
“Kwa hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe na tukijisimamia sisi wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake kwelikweli, kama ni mfanyabiashara afanye biashara kweli kweli, kama ni mfugaji afuge kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka,” alisema Rais Magufuli.
Alisema Serikali yake imeamua kuchukua hatua kudhibiti nidhamu serikalini, kwa kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi wa umma wanaolisababishia taifa upotevu mkubwa wa fedha, na ameahidi kuwa hatua hizo maarufu kwa jina la ‘Kutumbua Majipu’ zitaendelea kuchukuliwa hadi tatizo hilo likomeshwe.
Onyo kwa wateule
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli amewakumbusha viongozi wote wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi, kutekeleza wajibu wao ipasavyo na ameweka bayana kuwa mahali popote ambapo hapatakuwa na ufanisi, kiongozi husika atakuwa amedhihirisha kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa aliopewa.
Rais Magufuli, aliwapongeza walimu kote nchini kwa kufanya kazi nzuri ya kufundisha, licha ya changamoto ya ongezeko kubwa la wanafunzi waliojiunga darasa la kwanza mwaka huu,  ambapo aliwataka lwazazi na kamati za shule kushirikiana na walimu kuwasimamia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
“Niziombe kamati za shule zote Tanzania nzima, kama haziwezi kusimamia nidhamu ya wanafunzi shuleni, zile kamati za shule zijiuzulu.

“Lakini pia kama wewe ni mwalimu mkuu, shule yako kila siku inatoa divisheni ziro nyingi kila mwaka, sioni sababu ya wewe kuendelea kuwa mwalimu mkuu,” alisema Dk. Magufuli.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment