Image
Image

Wanaobainika kuwa ni watumishi hewa waondolewe mara moja ili kuinusuru Nchi.

SIKU 15 zilizotolewa na Rais John Magufuli kwa wakuu wa mikoa kujumlisha waajiriwa wa Serikali wote kwenye mikoa yao, kuwaondoa wafanyakazi hewa zilikwisha jana huku mikoa michache ikiweka wazi taarifa kamili kuhusu idadi ya wafanyakazi hao iliyoibaini.
Miongoni mwa mikoa hiyo na idadi ya wafanyakazi hewa kwenye mabano ni pamoja na Dodoma (144) na Kigoma (169). Mkoa wa Pwani ulikuwa mbioni kukamilisha uhakiki wake kwa lengo la kutoa taarifa hiyo jana, huku baadhi ya mikoa ambayo taarifa zake za uhakiki hazijawekwa bayana hadi sasa ikieleza kuendelea na utekelezaji wa agizo hilo la Rais.
Mikoa hiyo ni pamoja na Dar es Salaam, ambao baadhi ya wakuu wa wilaya zake wameamuru watumishi wote, hata walio masomoni na likizo, wawepo kazini ili kuhakikiwa. Rais Magufuli alifikia uamuzi wa kuwaagiza wakuu hao wa mikoa kuhakiki watumishi kutokana na taarifa aliyoipata kutoka katika mikoa ya Singida na Dodoma kuwa kuna watumishi hewa.
Inaelezwa kuwa, uchunguzi uliofanywa katika mikoa hiyo miwili yenye Halmashauri 14, ulionesha kuwa, kuna watumishi hewa 202 wanaoendelea kulipwa mishahara, hivyo kuisababisha Serikali hasara.
Wakati akiwaapisha wakuu hao wa mikoa, Machi 15, mwaka huu, Rais Magufuli alisema Serikali inatumia Sh bilioni 549 hadi Sh bilioni 550 kila mwezi kulipa mishahara ya watumishi wa umma. Rais alisema, inasikitisha kuona fedha zinazokusanywa haziendi kwenye miradi ya maendeleo inayopangwa, bali huishia kulipa mishahara hewa.
Alionya kuwa, itakapogundulika kuwa kuna mfanyakazi hewa katika orodha ya wanaostahili kulipwa mshahara mwezi ujao, mkurugenzi husika ajihesabu kuwa hana kazi, huku akisubiri kufikishwa mahakamani.
Ili kuonesha kuwa alimaanisha alichokisema huku akitegemea kuona utekelezaji ndani ya muda alioutoa, Rais Magufuli aliwataka Mawaziri hususan wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango aliyekuwepo wakati akiwaapisha wakuu hao wa mikoa, awaeleze watendaji kwenye wizara zao na taasisi mbalimbali wawaondoe watumishi hewa.
Inaelezwa kuwa, watumishi hewa katika mikoa mingi nchini ni wale ambao majina yao yameendelea kuwepo kwenye orodha ya malipo ya mishahara, ilhali ikijulikana kuwa wamefariki dunia na wengine kufukuzwa kazi.
Malipo hewa ni hasara kwa taifa, kwa sababu yanachangia kudumaza maendeleo katika sekta zinazohitaji fedha ili kukua au kuboreshwa. Baadhi ya sekta hizo ni ya afya na elimu, hasa ikizingatiwa kuwa wanafunzi wanatakiwa kugharamiwa na Serikali wapate elimu ya msingi hadi sekondari, ambayo ni ngazi ya kidato cha nne.

Tunawasihi viongozi wa mikoa ambayo taarifa za uhakiki hazijakamilika hadi sasa kutofanya mzaha ili kumsaidia Rais Magufuli kuhakikisha mipango yote ya maendeleo ya nchi yetu inafanikiwa. Ikumbukwe kuwa kuchelewa kutekeleza agizo hilo ni kuendelea kuitia hasara Serikali, kwa kuwa malipo ya wasio stahili yataendelea kuwepo kwenye orodha isivyo halali na kulipwa.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment