Image
Image

Serikali imeanzisha taasisi mbalimbali za umma ili kurahisisha utendaji kazi.

KATIKA kuhakikisha kwamba taifa linapiga hatua kubwa ya kimaendeleo na wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati, Serikali imeanzisha taasisi mbalimbali za umma ili kurahisisha utendaji na hatimaye utoaji wa huduma makini kwa wananchi.
Moja ya taasisi hizo ni Taasisi ya Miradi na Maendeleo ya Miundombinu, (UTT –PID) Hii ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha ambayo ilianza shughuli zake rasmi Julai Mwaka 2013. Ofisa Mtendaji Mkuu wa UTTPID Dk Gration Kamugisha anasema kuwa taasisi hiyo inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja. Anazitaja kazi kuu za UTT-PID kuwa ni utoaji wa huduma za ushauri katika maeneo ya Upembuzi yakinifu wa miradi mbalimbali, maandalizi ya hadidu za rejea, mipango ya huduma za kifedha, kuwasilisha miradi na huduma zinazohusiana.
Msingi wa kuanzishwa kwa taasisi hii na Serikali ni kuweka manzingira wezeshi ili kupata au kuvutia mtaji binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo sharti iwe inakidhi vigezo vya kuwa na faida za kijamii, kiuchumi na kifedha. Miradi mingi iliyotekelezwa hadi sasa inahusiana na uendelezaji wa ardhi na majengo lakini lengo na mtazamo wa taasisi ni zaidi ya hapo.
Ipo miradi mingi na mikubwa ya kimiundombinu katika sekta za afya, elimu na nishati, ambayo imeletwa kwenye taasisi na wadau mbalimbali hasa taasisi za umma ambayo inatafutiwa fedha. Dk Kamugisha anafafanua kuwa ili taasisi yoyote ile ipige hatua ni lazima iwe na Dira hivyo kwa upande wao Dira yao ni kuwa mdau wa maendeleo wa kuaminika katika fani ya Usimamizi wa Miradi na Maendeleo ya Miundombinu na kuwa na mtazamo wa uwajibikaji wa dhati ili kutosheleza mahitaji kwa wateja na kuendelea kuboresha huduma.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawajibika kwa wateja watu na katika hili ni lazima tutoe huduma bora ambazo zinakata kiu ya wateja wetu,” anasema. Anabainisha kwamba dhamira yao ni kufungua mitaji iliyodumaa kwa kuwasaidia wateja kitaalamu katika maeneo ya miradi na maendeleo ya miundombinu na kuleta ukuaji wa mapato kwa ajili ya wateja na wadau ambao ni pamoja mwanahisa (serikali).
Anasema wanapokwenda kupanga mji katika eneo lolote katika nchi yetu kwa mfano, ni wazi kwamba barabara zitachongwa, huduma za umeme zitafika, huduma za maji zitakuwepo, na shughuli nyingine za kiuchumi zinazoendana na huduma hizo zitafanyika. “Kwa hiyo utaona ni dhahiri kwamba wananchi watafaidika na huduma zinazotokana na uwezekezaji wetu katika eneo husika na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi,” anasema.
Lakini Dk Kamugisha anabainisha kuwa katika kufanikisha yote hayo ni lazima kuwe na maadili hivyo suala la maadili kwao ni kipaumbele kikubwa. “Tunaongozwa na misingi ya uwajibikaji, uwezo na motisha kwa wafanyakazi, uhakika wa ongezeko la wafanyakazi wenye sifa, kuthamini uvumbuzi, utambuzi na maboresho ili kuepuka au kupunguza uwezekano wa kujitokeza kwa malalamiko”.
Pia katika kutekeleza majukumu yao anasema suala la ubora wa huduma ni kipaumbele ambapo dhana nzima ya utoaji bidhaa /huduma zenye sifa na thamani ya kipekee kwa gharama nafuu. Anabainisha kuwa wamekuwa wakijitahidi kutoa huduma bora kwa wateja wao katika kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kulingana na thamani ya fedha na hivyo kumridhisha mteja.
“Tunajitahidi sana kukidhi mahitaji ya mteja, kuhakikisha kwamba taasisi inatoa huduma zilizo bora kwa wateja wao kwa kiwango kinachokidhi na hata kuzidi matarajio yao,” anasema Dk Kamugisha. Kuhusu suala la faida anasema taasisi yake imejikimu kimsingi katika uwezo wa kuongeza faida kutokana na uwekezaji wake kama vile kubadilika kulingana na mazingira ya kibiashara ili kufikia thamani ya huduma wanayoitarajia wadau wao.
Anaeleza kuwa wanafanya uratibu wa fedha na huduma zinazohusiana katika maandalizi na mapendekezo ya miradi kwa benki na taasisi za fedha, utambuzi wa mfadhili/wafadhili wa kifedha, kusaidia katika uthibitishaji wa nyaraka sahihi na ufatiliaji wa huduma ya mkopo. Tunafanya kazi ya usimamizi wa siku kwa siku wa miradi ya aina mbalimbali kama ujenzi upangaji miji, usimamizi wa majengo yaliyokwisha kamilika kwa maana ya kutafuta na kuhudumia wapangaji.
Usimamizi wa majengo na mali
Dk Kamugisha anasema wanajihusisha pia na utoaji wa huduma fanisi za usimamizi wa majengo yaliyo chini ya uangalizi thabiti wa taasisi, ukusanyaji wa kodi ya jengo kwa niaba ya mwekezaji /mwenye jengo. Kwa mfano mkoani Mbeya taasisi hiyo inasimamia uendeshaji wa Soko la Mwanjelwa ambalo limejengwa kwa ushirikiano baina ya benki ya CRDB na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
“Tunalisimamia soko lile vizuri kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi ambao ndiyo walengwa wanapata huduma bora na hivyo kusaidia katika kunyanyua hali zao za maisha na pia wakati huo huo kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Jiji inatimizia malengo yake,” anasema. Anasema kuwa UTT-PID, daima inashawishika kutoa huduma nyingine yoyote hususani katika upande wa miundombinu na uwekezaji katika sekta zote za kiuchumi.
Mafanikio ya taasisi mpaka sasa Anasema kuwa wamefanikiwa katika kuwezesha utekelezaji wa mradi wa Shirikisho la Vyama Vya ushirika Tanzania (TFC) Taasisi iliwezesha upatikanaji wa mtaji ambao ulitumika katika ujenzi wa jengo jipya la ghorofa 20 na ukarabati wa jengo la zamani. Pia kwa upangaji wa miji katika mkoa wa Lindi jumla ya viwanja 10,000 vya matumizi mbalimbali vinatarajiwa kupimwa.
Hadi sasa jumla ya viwanja 2,473 vimeshapimwa (awamu ya kwanza) kwa ufadhili wa Taasisi yetu ikishirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na wadau wengine wa maendeleo mkoani humo. Viwanja hivyo viliuzwa kwa utaratibu wa wazi kabisa kwa wateja mbalimbali kupitia Benki ya Posta.
“Ilikuwa haijawahi kutokea kwa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kupima viwanja vingi namna hii kwa wakati mmoja. Pamoja na viwanja hivi kuonekana ni vingi bado kuna wananchi waliokosa . Hii inaonesha jinsi ambavyo wananchi wanatamani kuishi katika maeneo yaliyopimwa na kupangiliwa vizuri,” anafafanua Dk Kamugisha. Anasema kuwa katika Wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza awamu ya kwanza katika Mradi huu taasisi kwa kushirikiana na Halmashauri iliwezesha upimaji wa viwanja 1,230 na uwekezaji wa baadhi ya miundombinu.
Kwa kushirikiana na Manispaa ya Bukoba, taasisi imefanikiwa upimaji wa viwanja karibu 5000. Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya Manispaa ya Bukoba, viwanja vilivyopimwa kwa ufadhili wa UTT-PID kwa wakati mmoja ni vingi kuliko viwanja vyote vilivyokuwa vimewahi kupimwa ndani ya manispaa hiyo tangu uhuru.
Kuhusu manufaa ya miradi hiyo, Dk Kamugisha anasema kwamba manufaa ni makubwa sana mathalani katika mkoa wa Lindi, utekelezaji wa mradi wa upimaji viwanja uliiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya kutekeleza miradi mbalimbali kutokana na fedha zilizopatikana kwenye mradi huo.
“Maabara zimejengwa katika shule za sekondari nyumba za walimu, boti inayotoa huduma kwa wananchi kati ya Lindi mjini na eneo la Kitunda,” anasema. Mradi huo umekuza shughuli za kiuchumi katika maeneo uliyoyapitia, mathalani, wa miundombinu kama vile ya barabara. “Hali hiyo imesababisha hata uchumi wa mwananchi mmoja mmoja kukua kwakuwa wanaweza kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo sanjari na mradi huo,” anafafanua.
Lakini pia faida nyingine ya miradi yao ya kupanga miji ni upatikanaji wa hati kwa wanunuzi ndani ya muda mfupi. “Utaona sasa wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali za kifedha kupitia hati hizo na hatimaye kujiletea maendeleo,” anasema. Baadhi ya wananchi wanaipongeza UTT-PID kwa kuendesha miradi mbalimbali ya upimaji ardhi na kiuchumi kwa ujumla kwani inachochea ukuaji wa uchumi.
“Mimi kwa kweli nawapongeza hasa kwa kupima viwanja kwani wamekuwa wakiwasaidia Watanzania hasa wale wa hali ya chini kuweza kupata hati ambazo zinawasaidia katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi,” anasema John Mwakatobe mkazi wa Gongo la Mboto, Ilala jijini Dar es Salaam. Anafafanua kuwa si rahisi kwa kila mtu hata kama ana fedha kuweza kufatilia hati kiwanja katika mamlaka husika kwa muda muafaka, lakini kwa kuwatumia taasisi ya UTT-PID ni jambo linalofanyika kwa muda mfupi sana.

Naye Ali Salehe, mfanyabiashara eneo la Mnazi Mmoja anawapongeza UTT-PID kwa kukarabati jengo la zamani la Ushirika na kujenga jengo jipya la kisasa ambalo limesaidia kuupendezesha mji. “Nawapongeza sana kwa kuupendezesha mji pamoja na kujenga jengo la kisasa eneo hilo ambalo lina shughuli nyingi za kiuchumi jambo ambalo linasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kuiingizia serikali mapato,” anasema.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment