Image
Image

Rais Magufuli atoa msamaha kwa wafungwa 3,551.


RAIS John Magufuli katika kusherehekea miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ametoa msamaha kwa wafungwa 3,551 kwa kuwapunguzia 1/6 ya vifungo vyao. Katika msamaha huo, wafungwa 580 wataachiwa huru huku wengine 2,971 wakinufaika na msamaha lakini watabaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira ilisema wafungwa wote wamepunguziwa 1/6 ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura 58 isipokuwa walioorodheshwa katika Ibara ya Pili.
Meja Jenerali Rwegasira alisema msamaha huo utawahusu wafungwa wenye magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu na saratani na wako katika hatua ya mwisho, wazee wenye miaka 70 au zaidi ambao magonjwa na umri viwe vimethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Alisema pia wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili ambao ulemavu huo umeidhinishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
“Ni mategemeo ya Serikali watakaoachiwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Alisema msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na wale wenye adhabu kama hiyo lakini imebadilishwa kuwa kifungo cha maisha. Pia wanaotumikia kifungo wa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kama cocaine, heroine, bangi na mengineyo na wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.
“Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi ukiwemo wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo, au wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isiyo halali,” ilisema sehemu ya taarifa ya Katibu Mkuu Meja Jenerali Rwegasira.
Alitaja wafungwa wengine ambao hawatahusika na msamaha huo ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo na wale wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment