Image
Image

SERIKALI:Kutokuoneshwa Matangazo ya Bunge LIVE hakuvunji Katiba.


SERIKALI imesema hatua ya kutotangazwa moja kwa moja kwa matangazo ya televisheni kutoka katika vikao vya Bunge mjini Dodoma hakuvunji Katiba, kama ilivyodaiwa na wapinzani wakati waliposusa mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Imesema kipengele kinachodaiwa kuvunjwa ndani ya Katiba kwa suala hilo ni Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo hata hivyo inazungumzia uhuru wa kupata taarifa.
Kifungu hicho kinasema: “Kila mtu (i)anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake, (ii) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi, (iii) anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake na (iii) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii”.
Kwa mantiki hiyo hakuna sehemu ya Katiba hiyo, inayotaka habari hizo lazima ziwe ‘live’. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju aliyasema hayo wakati akijibu hoja zilizojitokeza katika Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2016/17.
Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali alisema hoja hiyo ingekuwa na nguvu endapo waandishi wa habari wangezuiwa kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge kuchukua taarifa za mwenendo wa vikao vya Bunge.
“Ni jambo la aibu kwa wabunge kuacha kuchangia Bajeti ya Waziri Mkuu kwa vile tu eti hawaonekani kwenye televisheni. Tuwatumikie wananchi wetu ambao wametutuma. Haki ya kupewa taarifa si haki ya kutangazwa ndio maana huwezi kwenda mahakama yoyote kudai kwamba sijui mimi sijatangazwa,” alisema Masaju.
Kuhusu hoja kwamba Serikali imepoka madaraka ya Bunge, alisema hoja hiyo haina ukweli wowote kwa vile Bunge linaendelea kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia serikali ili itimize majukumu yake ipasavyo.
“Hoja kwamba serikali imepoka madaraka ya Bunge si kweli na wabunge hawapaswi kusema hivyo kwa sababu Bunge limepewa uhuru na haki ya kujadili haki ambayo haiwezi kupingwa na mahakama yoyote au kuhojiwa kwa mujibu wa Ibara ya 100,” alisema Mwanasheria Mkuu.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema mpango wa serikali kutaka Bunge kuwa na studio yake utasaidia kuwapunguzia gharama vyombo vya habari kuja Dodoma.
Nape alisema pamoja na mambo mengine mfumo huo utavisaidia vyombo vya habari kupunguza gharama ya kufika Dodoma kufuata taarifa na badala yake watakuwa wanapata taarifa moja kwa moja kupitia studio hiyo kwa bei nafuu na kuongeza kuwa kinachotakiwa sasa ni kwa pande husika kukaa na kuangalia upungufu uliopo ili kumaliza matatizo yaliyopo.
“Kwa tathmini tuliyoifanya wakati wa mkutano wa Bunge ulipokuwa ukioneshwa ‘live’, watu wengi mchana walikuwa hawafuatilii kwa wingi kama wanavyofanya hivi sasa, wakati kipindi cha Leo katika Bunge kinapooneshwa usiku,” alisema Nape.
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Malembeka (CCM) alisema kuna haja ya wabunge kupimwa akili kabla ya kuingia bungeni kutokana na baadhi yao kuonesha vitendo vinavyotia shaka.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) alisema anashangazwa na wabunge wa upinzani kudai kwamba serikali inavunja Katiba huku wao wakichukua posho wakati wamesusa. “Wanasema eti serikali imevunja Katiba lakini posho wanachukua.
Bunge lililopita akina Wenje (Ezekiah – aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana) na wenzake walipiga kelele hapa eti Kabwe (Willson – aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam) asimamishwe, leo Rais kamtumbua wanasema anakurupuka yaani hawa hawaaminiki, wanazungumza kila kitu,” alisema Lusinde.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment