Image
Image

Ukata watesa wabunge*Wapanga foleni kusotea posho kiduchu ya 30,000/-

MPANGO wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kufyeka baadhi ya posho kwa nia ya kubana matumizi, umeanza kuwaathiri wabunge wanaohudhuria kikao cha Bunge la 11 kutokana na ukata uliopitiliza, imefahamika.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa hivi sasa, baadhi ya wabunge wanaonekana kupunguza hata matumizi yao kwa kutoonekana mara kwa mara kwenye maeneo ya starehe waliyokuwa wamezoeleka ukilinganisha na siku za nyuma.
Aidha, dalili hizo za kuwapo kwa hali ngumu ya kifedha kulinganisha na vile ilivyokuwa kabla ya kuingia kwa utawala wa awamu ya tano, ni tukio lililojiri hivi karibuni mjini Dodoma wakati wabunge walipoonekana wakipanga foleni ndefu kusaini posho ya Sh. 30,000.
Tangu kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imekuwa mstari wa mbele kudhibiti matumizi ya fedha katika masuala yasiyowanufaisha wananchi moja kwa moja.
Lengo la serikali ni kuelekeza fedha zaidi kwenye miradi ya maendeleo inayonufaisha wananchi na kufanikisha ahadi mbalimbali ikiwamo ya utoaji wa elimu bure ulioanza tangu Januari, mwaka huu.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa ukata wa wabunge umetokana na kuondolewa mianya mingi ya kujiingizia fedha ikiwamo ya kudhibitiwa kwa safari za nje ya nchi na pia kuondolewa kwa posho katika vikao vya kazi vya kamati zao mbalimbali.
Pia wameondolewa posho walizokuwa wakisaini kila mara wanapokwenda kutembelea mashirika na taasisi mbalimbali za umma, achilia mbali vyakula na vinywaji tele walivyokuwa wakigharimiwa na Bunge wanapokuwa kwenye vikao vya kamati.
Hata hivyo, mpango huo wa serikali katika kubana matumizi umekuwa shubiri kwa baadhi ya wabunge waliokuwa wamezoea posho za vikao vya kamati na semina ambazo sasa zimefyekwa na kubaki historia.
FOLENI POSHO SH. 30,000
Katika hali isiyotarajiwa, Nipashe ilishuhudia siku za Jumamosi na Jumapili wiki iliyopita, wabunge waliohudhuria semina ya mafunzo ya uongozi kwenye ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya viunga vya Bunge mjini hapa, wakipanga foleni kusaini posho ya Sh. 30,000 na Sh. 45,000.

Semina hiyo iliyoandaliwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), ilihusu masuala ya uongozi bora na namna wabunge wanavyoweza kushiriki kuleta maendeleo.
Walengwa wa semina hiyo walikuwa ni wabunge vijana na wanawake, na mada zilitolewa na Mariam Sarungi, ambaye ni mdau wa masuala ya wanawake na urembo na Mbunge wa Jimbo la Kibra jijini Nairobi, Kenya (ODM), Ken Okoth.
Siku ya kwanza ya semina hiyo, wabunge waliohudhuria walipewa posho ya Sh. 30,000 ambazo walilipwa kwa utaratibu wa kupanga foleni na bahati mbaya fedha ziliisha kabla wabunge wote hawajalipwa hali iliyomlazimu ofisa aliyekuwa na jukumu la kuwasainisha kuwaahidi kuwalipa siku inayofuata.
Hata hivyo, waandaaji walishindwa kutimiza ahadi kwa kuwalipa wabunge wote waliohudhuria siku ya pili kama walivyoahidi jana yake baada ya kuishiwa fedha kwa mara nyingine, hivyo kulazimika kuwaomba radhi wabunge.
"Naomba mnielewe waheshimiwa wabunge… fedha tulizokuwa tumeandaa zimekwisha. Leo wamekuja wabunge wengi zaidi. Mtusamehe sana," alisema mmoja wa maofisa wa USAID aliyekuwa na jukumu la kugawa posho kwa wabunge.
Uchunguzi zaidi wa Nipashe ulibaini kuwa hivi sasa, kwa kiasi kikubwa wabunge hutegemea kipato cha uhakika kutoka katika malipo yao ya kila mwezi ya Sh. milioni 11, huku kati ya fedha hizo, mshahara ukiwa ni takriban Sh. milioni 3.6 tu huku kiasi kingine kinachobaki kikingizwa kwenye mfuko wa maendeleo ya jimbo husika.
Fedha nyingine katika malipo hayo ya kila mwezi hugharimia shughuli nyingine kama kulipia mshahara wa katibu na dereva wa mbunge, ziara za mbunge jimboni, matengenezo ya gari na machapisho ya nyaraka za mbunge.
Gazeti hili limebaini kuwa yapo baadhi ya makato hupunguza zaidi mapato ya mbunge na baadhi yake ni kulipia mkopo wa Sh. milioni 90 waliopewa kwa ajili ya kununulia magari huku nusu ya fedha hizo wakilipiwa na serikali na kiasi kinachobaki (Sh. milioni 45) wakilipa wenyewe kupitia mishahara yao.
"Mwanzoni mwa mwaka huu, wabunge walipewa mkopo wa Sh. milioni 90. Kati ya fedha hizo, Sh. milioni 45 ni ruzuku na Sh. 45 milioni zingine ni za kununua gari ambazo wanakatwa Sh. 800,000 kwenye mshahara wa kila mwezi."
Kwa upande wa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), makato huongezeka kutokana na kile kinachoelezwa kuwa hupaswa kuchangia sehemu fulani ya mshahara wao kwa ajili ya maendeleo ya chama chao.
WABUNGE WAKIRI MAMBO MAGUMU
Katika mahojiano na Nipashe kwenye viunga vya Bunge hivi karibuni, Mbunge wa Igunga (CCM), Dk. Dalali Kafumu, alikiri kwamba hivi sasa hali ya wabunge kifedha ni ngumu kulinganisha na vile ilivyozoeleka.

Dk. Kafumu aliongeza kuwa ubunge hivi sasa ni wa kuchapa kazi zaidi na siyo marupurupu mengi kama ilivyokuwa katika awamu iliyopita na sababu kubwa ni utekelezaji wa mpango wa kubana matumizi wa serikali ya awamu ya tano.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucia Mlowe, alisema kupungua kwa posho za vikao vya Kamati za Bunge kumechangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya wabunge kuyumba kifedha.
"Kama unavyofahamu, katika mabunge yaliyopita, kulikuwa na posho nyingi zikiwamo za vikao vingi vya kamati.
Kwa mfano, unapokuwa kwenye vikao vya kamati, ulikuwa unalipwa posho ya kawaida ya Bunge na pia posho ya kamati ambayo ilikuwa ikilipwa na taasisi mliyotembelea au wizara husika," alisema Mlowe.
Alisema hivi sasa hawalipwi tena posho ya vikao vya kamati pale kamati husika inapokuwa inakutana wakati Bunge likiendelea na hivyo wanachoambulia ni Sh. 220,000 tu kwa siku ambayo ni posho ya kawaida ya vikao vya Bunge.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Matiko, alizungumzia suala hilo kwa kifupi akisema: "Ndugu yangu… kama kuna Mbunge alikuja hapa bungeni (Dodoma) akijua kwamba ubunge ni dili (unalipa), basi ameumia."
MASHINE ZA VIDOLE
Uchunguzi zaidi wa Nipashe umebaini kuwa kufungwa kwa mashine za kielektroniki ili kutambua alama za vidole, ni sababu nyingine ya kuwaongezea ukata wabunge watoro kwakuwa hapo kabla walikuwa wakiandikiwa majina na wenzao kwenye kitabu cha Bunge cha orodha ya mahudhurio ili wapate posho za kila siku; jambo ambalo hivi sasa halipo tena.

Akizungumzia utendaji wa mashine hizo, Dk. Kafumu alisema: "Sasa ni lazima uingie mwenyewe bungeni na kuchukuliwa alama za vidole. Ile tabia ya kuandikiana majina na kusaini kwenye kitabu cha mahudhurio haipo tena. Sasa unaweka kidole asubuhi ili upate posho yako ya asubuhi na jioni huwa hivyo pia. Hakuna namna nyingine."
NAIBU SPIKA ANENA
Akizungumza na Nipashe hivi karibuni kuhusiana na madai ya kuwapo kwa ukata wa fedha kwa baadhi ya wabunge, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema haamini kuwa suala hilo linatokana na maamuzi ya serikali ya awamu ya tano katika kubana matumizi.

"Sidhani kama kuna tatizo la masuala ya fedha maana posho na mishahara ya wabunge haijabadilika. Bado ni ile ile," alisema Dk. Ackson.
Akilihutubia Bunge wakati akilizindua Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisema serikali yake itadhibiti safari holela za nje ya nchi ambazo ziligharimu serikali Sh. bilioni 356.3 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015.
Bunge ni miongoni mwa taasisi zilizoongoza kwa matumizi makubwa ya fedha na nyingine ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment