Image
Image

WACHUMI wazungumzia baadhi ya taasisi za fedha kutoza asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)

WACHUMI wamejitokeza na kuzungumzia hatua ya baadhi ya taasisi za fedha kutangaza kuanza kutoza asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wateja wao, wakisema benki zinao uwezo wa kuepusha mzigo huo kuangukia kwa walaji.
Katika hatua nyingine, wamesema endapo serikali itatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kwamba fedha zitakazokusanywa katika mpango huo mpya zitatumika kugharimia miradi ya maendeleo kama afya, maji, barabara na nyinginezo, siku chache zijazo wananchi hawatajali tena kama italipwa na wao au kampuni.
Hata hivyo, kampuni za simu na benki zimehadharishwa juu ya upandishaji gharama za huduma za fedha, zikiambiwa inaweza kufanya wananchi waanze kukwepa matumizi ya simu na benki katika kutuma fedha na taifa litaingia katika tatizo lingine la watu kufuata huduma wakiwa na lundo la fedha mifukoni.
Ufafanuzi wa wachumi hao, unatokana na hatua ya Benki ya Exim kutoa tangazo la kuanza kuwatoza wateja wake asilimia 18 ya VAT kwa kila muamala, watakaoufanya katika huduma yoyote, isipokuwa riba za mikopo kuanzia Julai mosi, mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili, G
avana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu alisema kuwa VAT ni kodi inayopaswa kulipwa na mtu wa mwisho yaani mlaji, lakini alisema wakala (benki/ kampuni za simu) anayekusanya kwa niaba ya serikali anaweza kuangalia namna ya kumpunguzia mzigo mlaji.
“Mabenki au kampuni za simu zinaweza kuangalia namna ya kuweka mikakati ya kuwapunguzia mzigo walaji katika kulipa kodi hii,” alisema Profesa Ndulu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Kitivo cha Uchumi, Profesa Haji Semboja alisema ingawa katika dhana ya kawaida, VAT hutakiwa kulipwa na walaji, hatua hiyo inaweza kutekelezwa vinginevyo kulingana na kanuni na miongozo inayotolewa na serikali katika kutekeleza sheria husika.
Profesa Semboja alisema ingawa
hadi sasa bado kuna utata juu ya ni nani hasa anapaswa kulipa kodi ya VAT katika huduma za fedha katika benki na mitandao ya simu, lakini kampuni na benki si lazima zisukumie mzigo huo kwa walaji wa mwisho bali zinaweza kubeba nusu na kuwaachia wateja nusu au hata kubeba mzigo wote.
“Katika hali ya ushindani wa kibenki na kampuni za simu uliopo sasa na katika kuvutia wateja zaidi, kampuni ya simu au benki inaweza kuamua kubeba mzigo huo wa VAT nusu na kuwaachia wateja nusu au hata kubeba mzigo mzima kutegemea na hali ya kibiashara kupitia Mpango wa Huduma za Kijamii,” alisema Profesa Semboja.
Alisema hata hivyo suala la nani anastahili kulipa kodi ya VAT katika huduma ya fedha inaweza kutoweka endapo elimu ya kutosha itatolewa kwa wananchi na kuwawezesha kufahamu kuwa kodi hiyo ndiyo inayotumika kutekeleza miradi ya maendeleo kama maji, afya, barabara na nyinginezo kama ilivyo duniani kote.
Kuhusu kiwango cha fedha kinachotakiwa kulipiwa VAT Profesa Semboja alifafanua; “Kwa unayenunua umeme Tanesco kupitia Tigopesa basi kuna fedha ambayo utaambiwa umekatwa na ambayo sasa itakuwa ndio mapato ya kampuni ya simu.Kama ni shilingi mia moja ndio mapato ya kampuni ya simu basi asilimia 18 ya mapato hayo ndiyo inayotakiwa kulipwa kama VAT kwa serikali. “Sasa kwa kawaida kampuni hizo zingetakiwa kulipa hiyo VAT lakini hakuna kampuni inaweza kutaka kupata hasara hivyo kwa vyovyote vile kama faida yake ni hiyo Sh 100 na si zaidi, basi watataka hiyo VAT ilipwe na mlaji mwenyewe, hawawezi kuchukua Sh18 ili wamlipie mteja maana watapata hasara na hicho ndicho walichokifanya Benki ya Exim katika tangazo lao,” alisema Profesa Semboja.
Hata hivyo, mchumi huyo alisema endapo VAT itakayotozwa itapandisha gharama za huduma za fedha, wananchi wataanza kukwepa matumizi ya simu na benki katika kutuma fedha na taifa litaingia katika tatizo lingine la watu kufuata huduma wakiwa na lundo la fedha mifukoni, hatua itakayosababisha madhara mengine kama foleni, urasimu, ujambazi na mengineyo kama ilivyokuwa zamani.
Akizungumzia utata huo, ofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambaye hata hivyo hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema pamoja na kwamba VAT ni kodi inayopaswa kulipwa na mlaji, lakini mamlaka inasubiri maelekezo ya utekelezaji wa sheria mpya ya fedha ili kujua namna itakavyotozwa.
“Baada ya kupata sheria na kanuni kutoka serikalini, tutatengeneza kitu kinachoitwa ‘practice notice’ (notisi ya utekelezaji) ambayo sasa itaeleza namna kodi hiyo ya VAT katika huduma za fedha iwe ni katika benki au kampuni ya simu itakavyokusanywa. Kwa sasa sheria ipo katika ngazi ya bunge bado kwa hiyo siwezi kuielezea zaidi,” alisema.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment