Image
Image

BreakingNews:Askari wa Mauaji ya Mwangosi Jela miaka 15.


                                                         Daud Mwangosi.
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa, imemhukumu kwenda jela miaka 15 askari polisi Pasficus Simon, kwa kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi.
Mwangosi aliuawa Septemba 2, 2012 eneo la Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa, baada ya askari kuzuia mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akisoma hukumu hiyo leo 27 Julai 2016 kwa zaidi ya saa moja, Jaji Paul Kihwelo, alisema katika kutoa adhabu hiyo mahakama ilipitia maombi ya pande zote mbili.
Alisema upande wa mashtaka ulitaka mshtakiwa afungwe maisha jela, huku upande wa utetezi ukitaka aachiwe huru kutokana na sababu mbalimbali alizotoa.
Alisema kuwa licha ya pande zote mbili kuvutana, kila mmoja akiegemea upande wake, suala la adhabu gani apewe mshtakiwa litabaki kuwa ni la mahakama kwa vile hukumu si suala la hesabu bali ni la sheria.
“Mahakama itajikita katika mambo   mbalimbali ikiwamo aina ya kosa, mazingira lilipotokea tukio, masilahi ya familia na masilahi ya taifa kwa ujumla,” alisema.
Jaji Kihwelo alisema mahakama hiyo iliangalia pia haki kwa vile adhabu huwa haitolewi   kulipiza kisasi, bali hutolewa kama onyo, funzo au kuikanya jamii kutokorudia kosa hilo, kwa sababu kwa kufanya hivyo atakuwa anavunja kanuni na taratibu za nchi, hivyo naye adhabu inaweza kumkuta.
Alisema kumwachia huru mshtakiwa kupitia sheria namba 38 kama wakili wa upande wa utetezi, Rwezeura Kaijage alivyoomba, haiwezekani, na si jambo la uungwana kwa vile kosa alilotenda mshtakiwa ni kubwa.
“Kuachiwa huru au kupewa adhabu nyingine, jamii huko nje itapoteza imani na mahakama ambayo ndiyo chombo cha mwisho kinachotegemewa katika kutenda haki.
“Kumfunga mshtakiwa kifungo cha maisha jela au kifungo cha muda mrefu kama walivyoomba Jamhuri, haitasaidia kurudisha uhai wa marehemu Daud Mwangosi.
“Tunajua machungu waliyopata familia ya marehemu na tunajua machungu watakayopata ndugu wa mshtakuwa baada ya adhabu kutolewa, lakini niseme tu mahakama itaangalia mizania na kuangalia adhabu gani inayomfaa mshtakiwa wa kosa hili,” alisema Jaji Kihwelo na kuongeza:
“Kosa lililotendeka ni kubwa, na marehemu aliuawa kifo cha kinyama ambacho hakielezeki. Na kwa kuwa mtuhumiwa alifanya uzembe na kusababisha kifo, kwa kuwa ameshatumikia miaka minne gerezani, mahakama inakuhukumu kifungo cha miaka 15 gerezani na upande wowote ambao unaona haki haijatendeka, unaruhusiwa kukata rufaa.”
Baada ya Jaji Kihwelo kutoa hukumu hiyo, baadhi ya askari walionekana hawakufurahishwa, huku wengine walionekana kumwaga machozi.
Wengine walifunika nyuso zao kwa mikono huku wengine wakikimbilia kumfunika kwa shuka mshtakiwa na kumzingira ili waandishi wa habari wasiweze kumpiga picha.


Akizungumzia hukumu hiyo huku machozi yakimmiminika na kushindwa kuzungumza kwa kirefu kutokana na kulia, mke wa marehemu, Itika Ruben Mwangosi (Pichani Hapo), aliishukuru mahakama na  waandishi wa habari kwa ushirikiano waliouonyesha kwake tangu kifo cha   mume wake hadi siku ya hukumu hiyo.


Rais wa Klabu za Waandishi Tanzania (UTPC), Deodatus Msokolo(Pichani hapo juu), alisema   adhabu iliyotolewa ni jambo la msingi kwa tasnia ya waandishi wa habari, ambayo dunia na Tanzania kwa sasa inajua kuwa Jeshi la Polisi lilimuua mwandishi wa habari kinyama.


Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliendelea kulaani hatua ya polisi kutumia nguvu kubwa kuwadhibiti wanahabari waliofika mahakama hapo   kuripoti kesi hiyo, huku wengine wakiwaelekeza waandishi kufanya kazi kama wanavyotaka wao (polisi).
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment