WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza kufukuzwa kazi na kufikishwa
mahakamani kwa watumishi wote wa Sekta ya Afya watakaobainika kula fedha
zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen na Mganga Mkuu
wa Mkoa huo, Dk John Gurisha kusimamia na kulinda fedha za CHF
zinazochangwa na wananchi na kuhakikisha zinatumika kama
zilivyokusudiwa.
Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi katika mkutano
wa hadhara kwenye Jimbo la Kwela, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga.
“Kitendo cha kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa lengo la kupata
huduma za afya kinawafanya wakate tamaa ya kuendelea kuchangia mfuko
huo. Kama wako watumishi wenye tabia hizo waache mara moja,”
alisisitiza.
Mbali na kutoa agizo hilo kwa uongozi wa Mkoa wa Rukwa, pia Waziri
Mkuu aliwataka wananchi kujiunga na CHF kwa sababu mfuko huo
utawawezesha kupata huduma za matibabu bure wao na familia zao katika
kipindi cha mwaka mzima.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema barabara ya kutoka Ntendo hadi
Muze yenye urefu wa kilometa 85 itajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze
kupitika kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati.
Akizungumzia ombi lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas
Malocha (CCM) la kutaka tarafa hiyo ya Mtowisa kuwa wilaya au
halmashauri, Waziri Mkuu anakwenda kulifanyia kazi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment