Aliyewahi
kuwa kada wa muda mrefu wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru amewaomba
marais wastaafu, Rais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuzungumza na
Rais John Magufuli ili aitishe kikao kati ya Serikali na Chadema kwa
ajili ya kusitisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Septemba Mosi.
Kingunge
ametoa kauli hii leo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mbele ya
waandishi wa habari wakati akiongelea mvutano kati ya Chadema na
serikali unaoendelea kwa sasa.
Chadema kimeingia kwenye mvutano
mkubwa na serikali kutokana na dhamira yake ya kufanya mikutano na
maandamano nchi nzima chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta
(Ukuta).
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alisisitiza kutoruhusu
maandamano na mikutano ya kisiasa na kuagiza kuwa, wanaotaka kufanya
mikutano wafanye ndani ya mipaka ya majimbo yao na si vinginevyo jambo
ambalo Chadema wanapinga.
Hali hiyo imeibua mtikisiko mkubwa nchini
huku kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, wanasiasa,
wasomi na wananchi wa kawaida wakitaka kupatikana suluhu kabla ya
Septemba Mosi, tarehe iliyopangwa kuanza maandamano na mikutano hiyo.
Kwenye
mkutano wake na wanahabari Kingunge anawalaumu viongozi wastaafu
wakiwemo marais pamoja na mawaziri wakuu kwa kukaa kimwa wakati huu
ambao nchi inatikishwa huku Katiba ya Jamhuri ikisiginwa.
Miongoni
mwa viongozi wanaolalamikiwa kutosikika ama kuchukua hatua zozote ili
kuilinda Katiba ni pamoja na Marais Wastaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi,
Benjamin Mkapa na Aman Abeid Karume (Zanzibar).
Viongozi wengine waliotajwa ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Cleopa Msuya; Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
“Mzee Mwinyi yupo kimya, Mkapa kimya, Warioba kimya, Cleopa Msuya kimya, Amani Karume kimya,” amesema Kingunge na kuongeza;
“Ukimya
huu unatokana na nini? Hawa wote waliwahi kula viapo vya utii kwa
Katiba. Mimi nahoji, wazee wenzangu vipi mnakuwa kimya? Nawaambia kuwa
mnachofanya si sawa.
“Naomba wazee wote tujitokeze kuhesabiwa katika hili la uvunjifu wa Katiba na sheria.”
Kingunge
ambaye alihamia Chadema akitokea CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana kutokana na kutoridhishwa na namna mchakato wa kumpata mgombea
urais kutoka chama hicho amesema, Chadema inatumia haki yake ya
kikatiba.
“Naomba Rais Magufuli, akubali kuitisha kikao na Chadema
ambacho pia wazee wastaafu watahudhuria, akifanya hivyo hata sisi wazee
tutawageukia Chadema na kuwambia wasitishe mpango wao wa maandamano,”
amesema.
Amesema kwamba, kibaya zaidi Jeshi la Polisi linaandaa
bunduki kwa ajili ya kupambana na raia ambao hawana kitu na kuwa, hali
hiyo haipaswi kuvumiliwa.
Mwanasiasa huo amesema, Chadema wameamua
kutetea haki yao ya kikatiba na kisheria kwa kufanyaa maandamano kote
nchini, na kina wafuasi wengi hivyo si jambo la kubeza.
“Upande wa
pili, lipo Jeshi la Polisi na watawala ambao wanaahidi kuwakabili. Kwa
bahati mbaya polisi na watawala hawatetei Katiba wala Sheria,” amesema.
Amesema
kuwa, Tanzania kwa sasa inakabiliwa na ombwe la uongozi na kwamba, nchi
imekosa watawala wenye sifa thabiti ya kuongoza taifa.
“Kwa hakika,
tatizo kubwa la sasa la nchi yetu ni ombwe la kiuongozi, kwasababu kama
ni watawala tunao kweli kweli, lakini tunachokosa ni watawala wenye
maarifa ya kiuongozi.
“Inashangaza kuona wazee wastaafu kukaa kimya wakati nchi inakabiliwa na tatizo linaloweza kutuangamiza.
“Upande
mmoja unanoa mapanga, unaanda bunduki kwa ajili ya kuchinja na kuua na
upande wa pili wapo raia tu, tena wasio na silaha zozote.”
Kingunge anasema, wananchi ambao serikali na Jeshi la Polisi wanajiandaa kupambana nao, wanalilia Katiba na sheria zifuatwe.
“Laiti
kama Chadema wangekuwa hawatetei Katiba na sheria, kungekuwa na kila
sababu ya kuwashughulikia, lakini kwa kuwa wanatetea Katiba na sheria,
kuna umuhimu wa kuyapa uzito madai yao,” amesema Kingunge.
Mwanasiasa
huyo amesema kuwa, mvutano wa sasa sio wa Chadema na serikali isipokuwa
ni suala la wananchi wote wa wenye mapenzi mema na taifa lao.
“Hili ni suala la kila mtu anayependa utawala wa Katiba, Sheria na Utawala Bora,” amesema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment