WAZEE wa Klabu ya Yanga juzi walionana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo kukodisha
timu kwa Mwenyekiti wao Yusuf Manji. Manji aliuomba mkutano mkuu wa
dharura wa Yanga akodishiwe timu hiyo kwa miaka kumi na kwamba atakuwa
akitoa asilimia 25 ya faida, lakini akipata hasara itakuwa ya kwake.
Suala hilo limezua mtafaruku na kuchukuliwa kwa mtazamo tofauti na
wanachama wa klabu hiyo waliogawanyika makundi mawili wanaokataa na
kukubali mpango huo.
Kikao hicho cha Makonda na Wazee wa Yanga kimekuja siku chache baada
ya Manji kutangaza kujiondoa kwenye timu na kujivua uenyekiti kwa kile
alichodai kuandamwa kutokana na mpango wake huo hasa baada ya Katibu wa
Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali kupinga mpango huo kwenye vyombo vya
habari.
Wazee hao wakiongozwa na Akilimali na Hashimu Mhika walitinga kwa
Makonda juzi na inaelezwa kuwa na kikao kizito ambacho kilianza saa
mbili na nusu asubuhi hadi jioni.
Kikao hicho kimekuja ikiwa ni siku moja baada ya kundi la vijana wa
Yanga kuvamia nyumbani kwa Akilimali na kutaka kumpiga kwa kile
walichodai kuwa mzee huyo anaivuruga Yanga kwa kauli zake.
Hata hivyo hakuna aliyekuwa ta yari kuzungumzia kikao hicho kati ya
Makonda na Wazee ikidaiwa kilichozungumzwa ni siri yao. Akizungumza na
gazeti hili jana Makonda alisema: “Ni kweli nilikuwa na kikao na wazee
wangu, sipaswi kusema tulijadili nini ila tumeongea mengi, tumeelekezana
kwa hiyo yanabaki kuwa siri kati yangu na wazee wangu”.
Kwa upande wa Akilimali akizungumzia jambo hilo alisema: “Yameshaisha
hayo, nimeamua kujishusha na kuomba radhi tusameheane, ulimi hauna
mfupa, niliteleza, nashukuru tumesameheana na yameisha”.
Inadaiwa Akilimali alimtumia mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini
Francis Kifukwe amuombee radhi kwa Manji ambapo Manji aligoma kumsamehe
mpaka pale atakapoomba kupitia vyombo vya habari ambavyo alitumia
kumkashifu kwa kumuita mkurupukaji.
“Manji ni jembe langu, namkubali, yaliyotokea ni mgongano tu wa
kawaida, tumeshawekana sawa, nimemuomba msamaha kijana wangu, yamekwisha
sisi sote tu wamoja,”alisema Akilimali akithibitisha kutakiwa kuomba
radhi kwenye vyombo vya habari.
Akizungumzia ombi la Manji kukodisha timu, mjumbe wa Bodi ya
Wadhamini Francis Kifukwe alisema: “Mchakato bado, kuna mambo mengi
ambayo yanaendelea tulieni, tukiwa tayari kila kitu tutaweka wazi,”
alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment