Image
Image

Plan International yatoa rai kwa Serikali kuanzisha Idara ya Kazi migodini.

Meneja wa Miradi wa Shirika la Plan International - Geita, Gratian Kweyamba akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya malengo ya Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto, kulia ni Mratibu wa Mradi huo, Maxmillian Kitigwa. Mradi huu wa miaka mitatu unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), unaratibiwa na Shirika la Plan International na kutekelezwa katika Wilaya 3 za Mkoa wa Geita............................................................................................................................
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO. Geita 
Shirika la Plan International limetoa rai kwa Serikali kuanzisha Idara ya Kazi katika maeneo ya migodi ili ishirikiane na wachimbaji wa madini kuhakikisha tatizo la ajira kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 linakoma.
Hayo yamesemwa leo mkoani Geita na Mratibu wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto wa shirika hilo, Maxmillian Kitigwa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya changamoto zinazoukabili mradi huo.
Kitigwa amesema kuwa katika Mkoa huo kuna changamoto nyingi zinazowakabili watoto lakini kukosekana kwa Idara ya Kazi katika maeneo ya migodi kunasababisha uvunjwaji mkubwa wa haki za watoto kwa kuwa watoto wengi wanakimbilia kufanya shughuli mbalimbali katika maeneo hayo ili kujipatia kipato.
”Sasa hivi Geita imeshakuwa Mkoa, na mkoa huu umezungukwa na migodi mikubwa hivyo Serikali inatakiwa kuweka Idara ya Kazi katika sehemu hizi ili kuzuia ajira za watoto pamoja na kukomesha unyanyaswaji unaofanywa kwa baadhi ya watu wanaofanya kazi huko”, alisema Kitigwa.
Mratibu huyo amewaomba wananchi wa Mkoa huo waache kutatua matatizo kiundugu na badala yake watoe ushirikiano kwa kuripoti matukio mabaya yanayofanyika katika maeneo yao na kuyafikisha katika ngazi ya mkoa ili yafanyiwe kazi.
Naye Meneja wa Miradi wa Shirika hilo kwa Mkoa wa Geita, Gratian Kweyamba amesema kuwa mradi huo unalengo la kuhakikisha watoto wanalindwa na kuondolewa katika mazingira hatarishi hivyo, Serikali isaidie katika kutatua changamoto hii na kuwarudisha watoto katika makuzi mazuri.
“Ingawa rasilimali tulizonazo ni chache kuliko mahitaji ya watoto lakini tunajitahidi kuwajengea uwezo Serikali na wadau mbalimbali ili waweze kushiriki katika kuimarisha mfumo mzima wa ulinzi wa watoto na kuwafanya wakuwe katika mazingira bora”, alisema Kweyamba.
Mradi huu wa miaka mitatu unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na Shirika la Plan International, unatekelezwa Mkoani Geita katika Wilaya za Chato, Geita na Nyan’ghwale ukiwa na lengo la kuondoa ajira hatarishi na vitendo vya ukatili kwa watoto wanaoishi karibu na maeneo ya migodi, umeanzishwa Novemba 2015 na utagaharimu jumla ya Euro 1,500,000 hadi kuisha kwake.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment