Image
Image

Saratani shingo ya kizazi hatari kwa waathirika wa VVU


MKURUGENZI wa Huduma za Afya kutoka Marie Stopes Tanzania, Dk. Joseph Komwihangiro, amesema wanawake wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, ni kundi ambalo lipo hatarini zaidi kuugua saratani ya shingo ya kizazi.

Dk. Komwihangiro alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akielezea maadhimisho ya miaka 40 ya taasisi hiyo ambayo yanatarajiwa kuambatana na utoaji vipimo na matibabu bure kwa hospitali zote za taasisi hiyo nchi nzima.
Alisema wanawake wenye maambukizi wanauwezekano wa kupata saratani hiyo kutokana na kushuka kwa kinga za mwili, hivyo inakuwa ni rahisi kunyemelewa na magonjwa mbalimbali.
Alisema kwa mujibu wa takwimu zinaonyesha wanawake wanauwezekano mkubwa zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi kuliko wale wasio na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Aidha, alisema katika kuadhimisha kwa miaka 40 ya Marie Stopes Tanzania watatao huduma bure kuanzia Novemba 2 mwaka huu kwa siku sita katika nchi nzima kwenye huduma za uzazi wa mpango na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi.
Alisema hospitali zao zote zitakuwa zinatoa huduma hiyo na kwa upande wa Dar es Salaam wamepanga kwa siku wanawake 400 kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi.
Alisema kuwa saratani ya shingo ya kizazi inaongoza katika saratani zote na asilimia 12 ya wanawake wanaweza kupata ugonjwa huo.
Dk. Komwihangiro alisema kwa tawimu walizozifanya kuanzia Januari mwaka huu waliwafanyia uchunguzi wanawake 30,365 kuhusiana na saratani ya shingo ya kizazi na asilimia sita walionekana na dalili za ugonjwa huo.
Alisema kutokana na ugonjwa huo kuonekana kuwa ni tatizo kubwa Marie Stopes Tanzania imeweka mikakati yake katika kuwasaidia wananchi ili kupata kipimo kwa gharama ndogo ya Sh. 2,000 pamoja na matibabu.
“Huwa tuna mashine za kisasa kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi ugonjwa huo na gharama ni Sh. 2,000 lakini tunapokwenda kwenye maadhimisho ya miaka 40 tutatoa bure huduma hiyo pamoja na kuwatibia wananchi,” alisema Dk.Komwihangiro.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Marie Stopes, Anil Tambay, alisema shirika hilo ambalo ni la kimataifa linajishughulisha na kutoa huduma za afya ya uzazi.
Alisema shirika hilo lilianzishwa mwaka 1976 na ifikapo Oktoba 31 wataadhimisha miaka 40 na mikakati yao ifikapo 2020 wanawake milioni 12 ambao ni wapya kutumia uzazi wa mpango.
“Tangu tulipojiwekea huu mkakati tayari tumefanikiwa kupunguza mimba zisizotarajiwa na maelfu ya vifo vinavyotokana na uzazi kwa akina mama vimepungua,” alisema.
Tambay alisema mwaka jana wanawake 447,617 walinufaika na huduma za uzazi wa mpango.
Alisema wamedhamiria kufanya kazi kwa ukaribu na serikali katika kutimiza mpango wa kitaifa wa kuongeza matumizi ya njia za uzazi wa mpango kutoka asilimia 32 kwa mwaka 2015 mpaka asilimia 45 ifikapo mwaka 2020 hasa kwa akina mama na wasichana.
Aidha alisema katika kuadhimisha miaka 40 ya Marie Stopes International imejipanga kuboresha huduma zake kuwafikia wananchi wa kijijini kwa huduma za uzazi wa mpango hasa kwa akina mama na vijana.
“Tunaahidi kuhakikisha asilimia 70 ya watakaofikiwa kwa kutumia njia za uzazi wa mpango ni wale watu maskini wanaoishi chini ya dola moja za Kimarekani kwa siku na asilimia 20 vijana chini ya miaka 20,” alisema.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment