Image
Image

Wakati umefika wakuchukua hatua,Saratani sasa ni tishio nchini.


KUNA taarifa za kitaalamu kwamba ulaji wa vyakula vyenye viambata vya kemikali hatari kiafya ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuwapo kwa kasi kubwa ya ugonjwa wa saratani nchini.

Sababu nyingine za kuenea zaidi kwa ugonjwa wa kansa zimetajwa kuwa ni za kimazingira na kibaiolojia ikiwamo wanaume kuwa na wapenzi wengi.
Hayo yalibainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa, kwamba idadi ya wagonjwa imeongezeka kwa asilimia 100 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita huku wengi wao wakiwa ni wanawake.
Alisema idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na kwamba kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka huu, kuna ongezeko kubwa.

Kwa mujibu wa Dk. Kahesa, taasisi sasa inapokea wagonjwa wapya wa saratani 5,000 kwa mwaka kutoka wagonjwa 2,000 mwaka 2005 na kwamba asilimia 60 ya wagonjwa wanaofikishwa katika hospitali yao ni wanawake na kati ya hao, asilimia 36 hukutwa wakiwa na saratani ya shingo ya kizazi.
Alisema watu wengi hupata magonjwa ya saratani kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za ulaji wa vyakula vyenye kemikali hatari pamoja na sababu za kimazingira.
Anataja sababu nyingine ya kuwapo kwa wagonjwa wengi zaidi wa saratani ni ongezeko la idadi ya watu nchini, athari za baadhi ya michubuko wanayoipata kinamama kwenye via vya uzazi na kutokana na kinamama kushiriki tendo la ndoa na mwanaume mwenye uhusiano na wanawake wengi.
Hata hivyo, licha ya kuwapo uwezekano wa kuwa na watu wengi zaidi wenye kukabiliwa na magonjwa ya saratani, Mkurugenzi huyo anasema ni asilimia 10 tu ya wagonjwa nchini kote ndiyo hufika hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.
Maelezo aliyoyatoa Dk. Kahesa yanaendana na hali halisi ilivyo kwa sasa kutokana na watu wengi kuathirika kwa ugonjwa wa saratani.
Kutokana na hali hii, tunaona kwamba kuna haja kwa mamlaka mbalimbali ikiwamo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuchukua hatua za haraka za kuutangaza ugonjwa wa saratani kuwa ni janga la kitaifa ili jamii ielimishwe sababu zinazousababisha na hatua za kujiepusha.
Tunasema hivyo kutokana na nguvu kubwa iliyowekwa zikiwamo fedha katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na kuwasaidia waathirika wa Ukimwi.
Ikiwa jitihada hizo zitafanyika na serikali ikashirikiana na asasi zizizo za kiserikali, ni dhahiri kwamba maambukizi ya ugonjwa huo yatapungua.
Kwa kuwa kuna baadhi ya sababu za maambukizi ya saratani ambazo zinaweza kuepukika, tunaishauri jamii kuchukua hatua kwa kuepukana nazo ili wabaki salama kwa kuzingatia kuwa ugonjwa huo hauna tiba ya uhakika.
Ni matumaini yetu kwamba serikali, wadau na jamii nzima watalichukulia tatizo hilo kuwa ni janga la kitaifa, ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi.
Aidha, ni matarajio yetu kuwa kutakuwapo ushirikiano wa pamoja katika kupeana taarifa kuhusiana na maambukizi ya saratani na namna ya kujiepisha nayo. Hatua zinahitajika kuchukuliwa haraka, vinginevyo litakuwa janga la kitaifa. Aidha, kuna haja kwa watu kwenda mapema hospitali pale wanapoona dalili za maambukizi.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment