Image
Image

Sh milioni 200 kutumika kuzifanyia ukarabati bandari ya Wete na Pemba.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imeanza kuchukuwa hatua kurudisha huduma za usafirishaji wa abiria katika bandari ya Wete, Pemba na kutumia Sh milioni 200 kwa ajili ya kufanya ukarabati katika hatua ya awali.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mohamed Ahmada alisema hayo wakati akijibu swali la mwakilishi wa Gando, Mariamu Thani aliyetaka kujua mipango ya kuifanyia ukarabati bandari ya Wete imefikia hatua gani hadi sasa.
Akifafanua Ahmada alisema, lengo la Serikali ni kuona bandari hiyo inafanya kazi zake kama ilivyokuwa zamani na kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaoishi mkoa wa Kaskazini Pemba wenye idadi kubwa ya watu.
Alisema juhudi zimechukuliwa ikiwamo ya kuzungumza na wahisani mbali mbali kufanya ukarabati bandari hiyo kwa kuongeza kina cha maji kwa ajili ya kuziwezesha meli kufunga gati hapo bila ya matatizo.
Hata hivyo, Ahmada hakuitaja kampuni gani au mfadhili yupi anayeifanyia ukarabati bandari hiyo, ambayo kwa sasa haitumiki kwa ajili ya kufunga gati meli zinazotoa huduma katika kisiwa hicho.
Huduma za usafiri wa abiria katika bandari ya Wete zimekwama kwa muda mrefu ambapo kwa sasa huduma za meli zipo katika bandari ya Mkoani Pemba.
Kitendo cha kuwa na huduma duni za usafiri wa abiria katika bandari ya Wete, kinalalamikiwa na wananchi wa mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo abiria wanaokwenda huko hulazimika kushuka bandari ya Mkoani na kuanza safari kwenda katika mkoa wa Kaskazini Pemba.
Bandari hiyo kwa sasa inatoa huduma za majahazi yanayoleta bidhaa mbali mbali kutoka katika mikoa ya Tanzania Bara ikiwamo Tanga.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment