Image
Image

Dirisha dogo la usajili, Yanga, Simba na Azam FC wahaha.

WAKATI dirisha dogo la usajili likifunguliwa leo, vigogo vya soka nchini vya Yanga, Simba na Azam FC vimeanza mchakato wa kuwatafuta wachezaji ili kuboresha vikosi vyao. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hiyo ni nafasi muhimu ya kujiimarisha kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga, Simba na Azam FC zinaonekana kuendelea kutazama kimataifa kwa kutafuta wachezaji wa kigeni katika nafasi tofauti katika kuhakikisha timu zao zinaendelea kutikisa ndani na nje ya nchi.
Wachezaji wanaotajwa hadi sasa kusajiliwa ni kiungo mkabaji Meshack Chaila wa Zesco United ambaye huenda akaingia mkataba wa miaka miwili ndani ya wiki hii.
Kwa mujibu wa tovuti ya Yanga jana, Chaila ameshamalizana na timu hiyo na yuko tayari kujiunga nao wakati wowote.
Ujio wa mchezaji huyo huenda ukawatimua baadhi ya waliopo, ambapo hadi sasa Yanga ina idadi ya wachezaji saba wa kigeni, isipokuwa bado hawajawekwa hadharani ni akina nani watakaotemwa.
Mchezaji mwingine anayetajwa ni Kipre Tchetche ingawa tovuti ya Yanga inasema mfuko wao usajili unasuasua, hivyo kuna uwezekano wa kumsubiri Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji aliyeko Marekani ili kuokoa jahazi.
Wachezaji waliopo hadi sasa ni Mzambia Obrey Chirwa, Wazimbabwe Donald Ngoma na Thaban Kamusoko, Mrwanda Haruna Niyonzima, Mrundi Mbuyu Twite na Amis Tambwe na Mtogo Vicent Bossou.
Pia, kuna wachezaji wazawa kama Malimi Busungu ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikosa namba huenda akabaki au kupelekwa kwa mkopo katika timu nyingine zilizoonesha nia ya kumhitaji ikiwemo Tanzania Prisons au Majimaji.
Kwa upande wa Simba ilianza mchakato wa kutaka kumrejesha mchezaji wao Emmanuel Okwi anayecheza soka la kulipwa Denmark. Mchezaji huyu anadaiwa kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza huko aliko hivyo, huenda akarejeshwa.
Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema Okwi atarudi kwenye dirisha dogo. Tayari Simba ilianza kampeni za kumrejesha Okwi kwa kusaka maoni ya wadau kwenye mitandao ya kijamii kama ni sahihi kumrejesha mchezaji huyo wa Uganda.
Pia, licha ya Kipa wao namba moja Vicent Angban kuwapa mafanikio hadi sasa, kumekuwa na maoni ya wadau kutoridhishwa na kiwango chake. Lakini bado haijawekwa wazi kama ni miongoni mwa wachezaji watakaotemwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alisema hivi karibuni kuwa kuna wachezaji watakaotemwa, lakini hakuwataja.
Tetesi zimewataja wachezaji wengine kama Shomari Kapombe na Kipre Bolou kuwemo katika mpango wa kusajiliwa na timu hiyo. Wachezaji hao kwa sasa wanatumikia Azam FC.
Simba ina wachezaji wa kigeni akiwemo Angban, Laudit Mavugo, Juuko Murshid, Fredrick Blagnon, Method Mwanjale na Janvier Bokungu.
Na Azam FC inaonekana kutoridhishwa na wachezaji wake wa kigeni waliokuwepo, kwani tayari imeanza majaribio kwa wengine waliomiminika kusaka nafasi ya kucheza katika timu hiyo.
Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT Ruvu juzi, kulikuwa na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo mabeki wa kati Nkot Mandeng Eric (Coton Sport De Garoua, Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Asec Mimosa, Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Coton Sport Garoua, Cameroon).
Washambuliaji ni Yaya Anaba Joel (Coton Sport Garoua, Cameroon), Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Bernard Ofori (Medeama, Ghana) na Konan Oussou (Tala’ea El-Gaish SC, Misri).
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment