MAKAMU wa Rais mstaafu, Dk Mohammed Gharib Bilal ameonya kuwa uvuvi
wa haramu unaofanywa na wavuvi katika maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi
unatishia kutoweka kwa matumbawe, jambo ambalo lina madhara makubwa ya
kimazingira kwa nchi.
Akitoa mhadhara katika kongamano la mazingira na mabadiliko ya
tabianchi lililoandaliwa na kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Bilal alisema kitendo cha kuendesha uvuvi haramu
kunaharibu matumbawe ambayo yana umuhimu makubwa katika fukwe na viumbe
vingine vya baharini.
Dk Bilal alisema kama hatua za haraka hazitachukuliwa kudhibiti uvuvi
haramu wa kutumia baruti, janga kubwa la kimazingira litatokea na hivyo
kuathiri shughuli za kiuchumi na ustawi wa jamii, kwa vile matumbawe
hivi sasa yana faida kubwa katika nyanja hizo.
Katika mhadhara wake, Dk Bilal alisema uchafuzi wa mazingira kwa sasa
unatisha kutokana na watu wengi kutaka kutumia vyanzo vya mapato kwa
kuharibu mazingira, hivyo akasema kuna haja ya wadau wote kuunganisha
nguvu kukomesha athari za uhabirifu wa mazingira.
“Natoa mwito kwa wananchi wote, wawe wasikivu kwa ushauri unaotolewa
na wataalamu wetu wa Mazingira, tusipochukua tahadhari ya kutunza
mazingira vizazi vijavyo vitapata shida,” alisema Dk Bilal na kusisitiza
kuwa uvuvi huo haramu unakimbiza samaki, lakini pia unaathiri maisha ya
watu ambao uchumi wao unategemea rasilimali za baharini.
Katika hotuba yake, pia makamu huyo wa rais mstaafu alitaka
kukomeshwa ukataji wa mikoko kwani kufanya hivyo kunatishia uhai wa miti
hiyo ambayo huzuia kasi ya maji ya bahari kuvamia nchi kavu.
Alisisitiza kuwa ukataji wa mikoko una athari kubwa kwa nchi kwani
unasababisha mafuriko na mmonyoko wa udongo katika maeneo ya pwani ya
bahari.
Kongamano hilo la siku tano linahusisha washiriki kutoka nchi
mbalimbali ambao wanajadili namna ambavyo Afrika inaweza kupambana na
athari za mabadiliko ya nchi. Kongamano hilo lilifunguliwa juzi na
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alitaka wananchi wakomeshe
vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment