JUZI na jana Rais John Magufuli amekuwa Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Uhuru Kenyatta.
Tunampongeza Rais Magufuli kwa kufanya ziara hiyo katika taifa hilo
jirani, hasa kwa kuzingatia alikuwa hajaenda huko tangu aliposhika
madaraka mwezi Novemba mwaka jana. Tumevutiwa na kauli ya Rais Magufuli
ya kuwakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya, kuja kuwekeza
nchini, kutokana na jinsi wawekezaji wa nchi hiyo wanavyojitahidi
kuwekeza.
Mathalani, kwa mujibu wa Rais, Kenya ni nchi inayoongoza kwa
uwekezaji Tanzania, ikilinganishwa na nchi zote zaidi ya 50 za Bara la
Afrika. Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa
Kenya ina jumla ya kampuni 529 zinazoendesha shughuli zake Tanzania,
ambapo zimewekeza dola za Marekani bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.
Pia, biashara kati ya Tanzania na Kenya, imeongezeka kutoka shilingi
za Tanzania bilioni 652.9 hadi Sh trilioni 2.044. Rais Magufuli ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), aliwahakikishia
Wakenya kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kukua
zaidi.
Kwa miaka mingi, nchi hizi zinashirikiana vizuri katika uchumi.
Wakenya na Watanzania wanafanya kazi pamoja na yapo makabila yetu ambayo
yanaingiliana kwa tamaduni na shughuli zao za kila siku. Hata
wanyamapori wanazunguka katika nchi hizi mbili, bila kujali mipaka
iliyopo.
Tunampongeza Rais Magufuli kwa kusisitiza kuwa serikali ya Tanzania,
itaendelea kuimarisha zaidi uhusiano wake na Kenya, ulioasisiwa na Rais
wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa
Kenya, Mzee Jomo Kenyatta. Kwa miaka mingi, Watanzania na Wakenya
wanaguswa na kuthamini kazi kubwa, iliyofanywa na waasisi hao.
Kuhusu maendeleo ya Tanzania, Rais aliwaeleza Wakenya kwamba viongozi
wa serikali yake, wanaendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhimiza
ulipaji kodi na mapambano dhidi ya ufisadi. Kwamba, amekuwa akitumia
msemo wake wa ‘Hapa Kazi Tu’, unaohamasisha kila mtu kufanya kazi kwa
haraka ili nchi isonge mbele.
Pia, tunampongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kumhakikishia Rais Magufuli
kuwa Kenya itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na
Tanzania. Uhuru alibainisha kwamba kwa Wakenya, Watanzania ni ndugu zao,
kaka na dada zao wanaoshirikiana nao siku nyingi. Kwamba wataendeleza
ushirikiano na uhusiano huo mzuri, ulioasisiwa na wazee wetu hao.
Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu,
ikiwemo kubadilishana uongozi wa serikali kwa njia ya amani. Kwa
Tanzania, Nyerere alikabidhi kijiti kwa Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambaye
naye alimwachia Benjamin Mkapa.
Mkapa alipomaliza miaka yake kumi, alimuachia Jakaya Kikwete ambaye naye alikabidhi kijiti mwaka jana kwa Rais Magufuli.
Kwa upande wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta alimuachia madaraka Daniel
Arap Moi, ambaye alikabidhi kijiti kwa Mwai Kibaki, ambaye naye
alipomaliza muda wake alimwachia Uhuru Kenyatta. Hivyo, kama alivyosema
Rais Magufuli, tunawakaribisha wawekezaji wengi zaidi kutoka Kenya, waje
kuwekeza. Karibuni Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment