RAIS John Magufuli na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wamezindua
barabara ya Southern By-pass iliyojengwa kwa lengo la kupunguza
msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi, nchini Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Tanzania, sherehe ya uzinduzi wa
barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 28 na inayounganisha maeneo
mbalimbali ya Jiji la Nairobi, imefanyika katika eneo la Kareni nje
kidogo ya Jiji la Nairobi jana.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Magufuli amempongeza Rais
Kenyatta na serikali yake kwa kujenga barabara hiyo ambayo sio tu
itawasaidia wananchi wa Kenya, bali pia itawasaidia wananchi wa Afrika
Mashariki wanaotumia barabara zinazopitia Nairobi.
Rais Magufuli pia ameishukuru Serikali ya China kupitia benki yake ya
Exim ambayo imetoa mkopo wa kujenga barabara hiyo, kwa kuendelea
kuziamini nchi za Afrika Mashariki na kuzikopesha mikopo inayosaidia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.
“Wananchi wanahitaji maendeleo na haya ndio maendeleo, barabara hii
itasaidia kuinua uchumi na itasaidia masuala ya kijamii,” alisema Rais
Magufuli.
Dk Magufuli alisema viongozi wa Afrika Mashariki wameamua kufanya
kazi ya kuharakisha maendeleo na kuinua maisha ya wananchi, na kwamba
ili kufanikisha hilo wamedhamiria kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo
ujenzi wa barabara zinazounganisha nchi wanachama na kujenga vituo vya
pamoja vya utoaji wa huduma za mpakani.
Rais Kenyatta alisema kujengwa kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza
msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi na pia kutaboresha shughuli
za maendeleo ya wananchi.
Alimshukuru Rais Magufuli kwa kuungana naye kuzindua barabara hiyo na
alisema Kenya itaongeza juhudi katika utekelezaji mradi wa ujenzi wa
barabara zinazounganisha Kenya na Tanzania zikiwemo barabara ya Malindi
kupitia Saadani hadi Bagamoyo nchini Tanzania na barabara ya Voi -
Taveta- Holili-Arusha.
Sherehe za uzinduzi wa barabara ya Southern By-pass zilihudhuriwa na
Naibu Rais wa Kenya, William Ruto. Kabla ya kuzindua barabara hiyo, Rais
Magufuli alitembelea kiwanda kidogo cha kusindika maziwa cha Eldoville
kilichopo katika eneo la Karen ambacho kinamilikiwa na familia ya
mkulima James Karuga.
Familia hiyo ilianzisha kiwanda cha kusindika maziwa mwaka 1985 kwa
uzalishaji wa chini ya lita 1,000 kwa siku na hivi sasa imefikia
uzalishaji wa lita 5,000 kwa siku na inatarajia kuongeza uzalishaji hadi
lita 70,000 katika mwaka mmoja ujao baada ya kuongeza kiwanda cha pili.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment