Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kujenga Mahakama 40 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuongeza ufanisi na kuharakisha hukumu za kesi katika ngazi mbalimbali nchini.
Kutokana
na fedha itakayotumika kujenga mahakama, shilingi bilioni 36 zinatokana na
Bajeti ya mwaka huu wa fedha wakati shilingi bilioni 12.3 zilitolewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.
Hayo
yamebainishwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dkt.
Harisson Mwakyembe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iramba Mashariki Mhe.
Allan Kiula aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi
wa Mahakama za Wilaya na uteuzi wa Mahakimu katika ngazi hiyo.
Waziri
Mwakyembe amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Mahakama zinakuwepo kila
wilaya ili kuwaondolea usumbufu wananchi, kurahisisha usikilizwaji wa kesi
pamoja na kupunguza gharama kwa wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine
kufuata Mahakama zilipo.
“Kwa
mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria na Kanuni inaeleza kuwa kila Mahakama ina
mipaka yake hivyo hatuwezi kubadilisha mahakama ya mwanzo kutumika kama ya
wilaya” amesema Dkt. Mwakyembe.
Ameongeza
kuwa mpaka sasa bado kuna wilaya zinapata huduma ya Mahakama kupitia wilaya
nyingine ambapo amewahakikishia Wabunge na wananchi kuwa Serikali itajenga
mahakama 40 kwa mwaka huu wa fedha.
Akifafanua
mgawanyiko wa Mahakama 40 zinazotarajiwa kujengwa nchini, Dkt. Mwakyembe
amesema kuwa Serikali itajenga Mahakama Kuu nne, Mahakama za mikoa sita,
Mahakama za Wilaya 14 na Mahakama za Mwanzo 16 katika wilaya mbalimbali nchini.
Aidha,
Mhe. Mwakyembe ametaja baadhi ya vigezo vinavyotumika kuanzisha Mahakama katika
eneo lolote kuwa pamoja na uwepo wa hati ya kisheria ya kuwepo kwa wilaya,
mkoa, kata na kijiji, umbali wa upatikanaji wa huduma za Mahakama, idadi ya
wakazi wa eneo husika pamoja na uwepo wa huduma
zingine za kipolisi na magereza.
Ameongeza
kuwa kutokana na changamoto hizo za kukosekana kwa mahakama katika maeneo
ambayo yamekidhi vigezo ndiyo yaliyopelekea Serikali kujipanga kujenga Mahakama
hizo ambapo ametoa rai kwa wananchi kuwa na subira wakati wakikusubiri kujengwa
kwa Mahakama hizo.
0 comments:
Post a Comment