Image
Image

Sampuli za ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia panya buku wazinduliwa.

MAABARA ya kupima sampuli za ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kwa kutumia panya buku wa Mradi wa Apopo ulio chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), imezinduliwa jijini Dar es Salaam, huku ikielezwa kuwa panya mmoja ana uwezo wa kupima sampuli 100 ndani ya dakika 20.
Uzinduzi wa maabara hiyo ulifanywa jana na Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya wa Wizara ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mohamed Mohamed kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo na uzinduzi ulioshuhudiwa na wadau mbalimbali pamoja na wananchi.
Akielezea mradi huo wa kupima vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia panya waliofunzwa, Meneja Mradi, Dk Georgies Mgode alisema panya hao wana uwezo wa kubaini harufu ya vimelea vya ugonjwa huo ndani ya sekunde.
Aidha, alisema kwa dakika 20 panya anaweza kupima sampuli 100 wakati sampuli kama hizo zingepimwa kawaida kwenye maabara zinazotumia hadubini kwa siku nne, hivyo majibu hadi yafike kwa mgonjwa yanaweza kuchukua siku saba ili hali kwa kutumia panya mgonjwa ndani ya siku moja anapata majibu na kuanza tiba.
“Ni kweli hawa panya wana faida kubwa kwenye ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa wa TB, kwa sababu wana uwezo ndani ya sekunde wakabaini maambukizi ya kwa mgonjwa wakati mtu wa maabara anatumia zaidi ya siku moja kupata majibu,” alisema Dk Mgode.
Alisema kwa kuzinduliwa kwa maabara hiyo itakayokuwa na panya buku 10 jijini Dar es Salaam ni hatua ya mafanikio ya harakati za vita dhidi ya ugonjwa huo hasa kwa kuwa jiji hilo ndilo linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, kuliko maeneo mengine na pia ni moja la miji yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa kikua kikuu.
Akielezea jinsi panya hao wanavyofanya kazi, Dk Mgode alisema katika mradi wa Apopo panya hao walifanyiwa utafiti na wakagundulika kuwa na vinasaba vingi kuliko mnyama mwingine na ubongo wao una uwezo mkubwa wa kubaini vitu wakifundishwa.
Alisema kutokana na nchi kuwa miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi ya juu ya ugonjwa huo, kutumia njia ya hadubini kwenye maabara pekee hakutoshi katika kupambana na ugonjwa huo, na kuwa njia hiyo inatoa uhakika wa sampuli kwa asilimia 20 hadi 60 huko asilimia 40 hawagunduliki na hivyo kuendelea kuambukiza wengine.
Alisema kwa kutumia panya buku, wana uwezo wa kutambua harufu ya vimelea vya kifua kikuu, tofauti na vipimo vya kawaida vinavyotumika hospitalini ambavyo ni lazima vimelea vya ugonjwa huo vionekane kwenye darubini, jambo ambalo wakati mwingine ni vigumu kubaini vimelea hivyo iwapo mgonjwa hakuonesha dalili yoyote ya ugonjwa.
Alisema katika mradi huo, maabara nyingine ya panya buku iko Morogoro ambayo hutumika kupima sampuli mbalimbali kutoka hospitali 28 nchini ambazo hupeleka sampuli za wagonjwa na tangu mradi huo uanze kazi mwaka 2008 zaidi ya sampuli 380,000 zimeshapimwa kutoka hospitali mbalimbali nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua maabara hiyo, Dk Mohamed alisema hiyo ni hatua kubwa ya kuokoa maisha ya watu na kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo ambao changamoto kubwa ilikuwa kwenye upimaji kubaini vimelea wa ugonjwa huo.
“Hii ni hatua kubwa tunapongeza juhudi hizo za kuunga mkono serikali harakati za kupambana na ugonjwa wa TB, kwa sababu wakati mwingine hadi kuugundua ugonjwa ilikuwa vipimo kama kuotesha sampuli vifanywe na majibu yalichukua hata wiki sita, sasa utaona jinsi ugonjwa ulivyokuwa ukienea”, alisema Dk Mohamed.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP), Dk Allan Tarimo alisema Tanzania ni moja ya nchi zenye maambukizi ya juu ya ugonjwa wa kifua kikuu na katika takwimu barani Afrika inashika nafasi ya nne huku kimataifa ikiwa nafasi ya sita.
Dk Tarimo alisema pamoja na kuwa ugonjwa huo unatibika mgonjwa anapowahi kupata tiba, lakini hadi sasa ni kati ya wagonjwa 165,000 wanaogundulika kwa mwaka, wanaopata tiba ni chini ya wagonjwa 62,000.
Alisema kwa mujibu wa muongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa siku moja mtaalamu wa maabara anatakiwa kupima wagonjwa 20 tu wa kifua kikuu, ila kwa kutumia panya hao, kwa dakika 20 wanaweza kupima sampuli 100, na hiyo inakuwa mkombozi kwa kupunguza tatizo hilo, kama sio kuliondoa.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Magonjwa ya Mifugo (TVLA), Dk Furaha Mramba alisema mradi huo na maabara hiyo itakuwa mkombozi kutokomeza ugonjwa huo nchini.
TVLA wametoa eneo lililojengwa maabara hiyo jijini Dar es Salaam ili kusaidia kupambana na ugonjwa huo na kwamba watafiti wa mradi huo wa Apopo wanafanya kazi na watafiti kutoka TVLA.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment