"Uhusiano ni mkubwa kati ya matokeo ya kujifunza na utapiamlo, Twaweza inatoa mwito kwa wazazi na shule kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni," ulisema utafiti huo, ambao ulitangazwa jana na Twaweza kupitia programu ya Uwezo. Takwimu za utafiti zilikusanywa kati ya Oktoba na Desemba 2015 kutoka kwa watoto 197,451 na kaya 68,588.
Utafiti huo unaonesha kuwa uhusiano kati ya matokeo ya watoto ya kujifunza na utapiamlo, miongoni mwa watoto wenye miaka 10 mpaka 14 kwa upande wa somo la Kingereza, uwezo wa kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la 2 ilitofautiana.
Kiwango kilionesha kuwa watoto wenye utapiamlo, walifaulu kidogo wakati wale ambao hawana utapiamlo walifaulu zaidi.
Asilimia 17.9 ya watoto wenye utapiamlo walifaulu, wastani wa asilimia 16.4 ya watoto wenye utapiamlo wa wastani walifaulu, lakini watoto wasio na utapiamlo asilimia 25.8 walifaulu kusoma hadithi ya kiingerza ya darasa la pili.
Kwa upande wa somo la Kiswahili, uwezo wa kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la 2, watoto wenye utapiamlo (asilimia 46.3 walifaulu), watoto wenye utapiamlo wa wastani ( asilimia 51.3 walifaulu) na watoto wasio na utapiamlo ( asilimia 65.8 walifaulu).
Ripoti inaonesha kuwa katika somo la Hisabati, uwezo wa kufanya hesabu za kuzidisha za kiwango cha darasa la 2, watoto wenye utapiamlo ( asilimia 35.5 walifaulu), watoto wenye utapiamlo wa wastani ( asilimia 37.7 walifaulu) na watoto wasio na utapiamlo asilimia 53.4 walifaulu.
Matokeo haya yalitolewa jana na Twaweza katika hafla iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hafla hiyo ni sehemu ya mfululizo wa semina za Jielimishe, zinazofanyika kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu na Twaweza.
Meneja wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla, alisema hali ya lishe ya watoto, ina madhara kwenye kusoma Kiingereza ukilinganisha na Kiswahili na Hisabati.
Habari njema ni kwamba suala hili linaweza kujadiliwa, na watoto wanaweza kupatiwa chakula shuleni. Utoaji wa chakula shuleni unaweza ukawa njia mojawapo ya kuwapa motisha wanafunzi kuhudhuria zaidi shuleni.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema uwezo wa watoto kufanya vizuri shuleni, unaathiriwa na jinsi wanavyopata lishe nzuri. Aliongeza kuwa katika awamu hii ya elimu bila malipo ya ada, suala la utoaji wa chakula shuleni limeachwa njia panda.
"Halijaainishwa kwenye fedha za ruzuku zinazotumwa moja kwa moja shuleni na serikali. Wazazi nao wameacha kutoa michango shuleni, kutokana na matamko rasmi ya kufuta michango yote mashuleni. Je, suala la michango ya wazazi kwa ajili ya chakula cha watoto wao wakiwa shuleni bado halizungumziki," alisema Eyakuze.
Twaweza ilisema kuwa takwimu zilizokusanywa, zinaonesha kuwa kitaifa asilimia 4 ya watoto wenye umri chini ya miaka 5, asilimia 5.6 ya watoto wenye miaka kati ya 5 na 9 na asilimia 5.7 ya watoto wenye miaka kati ya 10 hadi 14 wana utapiamlo.
Utafiti huo ulifafanua kuwa hata hivyo kuna utofauti mkubwa kiwilaya, kwani kwa Songea Mjini asilimia 23.9 ya watoto walio chini ya miaka 5 wana utapiamlo, ukilinganisha na asilimia 0.3 ya watoto wa wilaya ya Tabora Mjini na Musoma Mjini.
Pia utafiti umebaini kuwa wastani, asilimia 50 ya kaya zinamudu milo mitatu kwa siku na matokeo ya utafiti, yanaonesha kuwa baadhi ya wilaya zina zaidi ya asilimia 85 ya kaya zinazomudu milo mitatu kwa siku. Wilaya hizo ni Mbulu asilimia 97.6, Kishapu asilimia 88.2, Mafinga Mjin asilimia 88, Tunduma asilimia 86.4, Moshi Mjini asilimia 86.
Katika wilaya nyingine, kaya chini ya asilimia 40 ndizo zinazomudu milo mitatu kwa siku nazo ni Masasi asilimia 38.6, Tandahimba asilimia 35.5, Mtwara Vijijini asilimia 27.6 na Nanyumbu – asilimia 23.1.
Kitaifa, ni shule moja tu kati ya tano inayotoa huduma ya chakula cha mchana shuleni (asilimia 23). Kwa mkoa wa Kilimanjaro, asilimia 79 ya shule zinatoa chakula cha mchana, lakini katika mkoa wa Geita, ni asilimia 5 tu ya shule zinazomudu chakula cha mchana kwa watoto.
0 comments:
Post a Comment