Image
Image

Maendeleo ya nchi yoyote yanategemea nguvu kazi ya vijana.

Maendeleo ya nchi yoyote yanategemea nguvu kazi ambayo kwa asilimia kubwa inatokana na vijana walioelimishwa na kupatiwa stadi mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Serikali inafanya juhudi kubwa katika kuhakikisha vijana wanapata ajira na wengine kujiajiri kwa kufanya kazi mbalimbali zikiwemo za kujenga viwanda, kuanzisha miradi ya kuwapatia wenzao ajira ikiwemo ya kilimo, mifugo, biashara ndogondogo pamoja na ujasiriamali.
Sio kazi ya Serikali pekee bali ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu na mafunzo ya kutosha ili waweze kujiajiri au kuajiriwa na hatimaye kupunguza utegemezi.
Hivyo Mashirika na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zinatakiwa kuhakikisha zinashirikiana na Serikali katika kuwapatia vijana ajira na elimu ya kujitegemea kwani ukuzaji wa ajira kwa vijana ndio kipaumbele kikubwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde anasema kuwa Serikali ya awamu ya tano imejipanga kukuza ujuzi wa nguvu kazi kwa vijana ambao utatolewa kupitia programu maalum ya mafunzo kazini kwa njia ya Uanagenzi (Apprenticeship), mafunzo kwa vitendo  kwa wahitimu (Internships) pamoja na urasimishaji  wa ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi (Recognition of Prior Learning).
Mhe. Mavunde anakakaririwa akisema kuwa, “Serikali yetu imetoa kipaumbele cha juu katika kujenga ujuzi wa nguvu kazi, takribani vijana 15,000 watafaidika na programu hiyo kwa mwaka huu wa fedha kwani tayari tumeanza kutekeleza kwa kuingia mikataba na Makampuni ya kutoa mafunzo kwa vitendo katika maeneo ya kazi”.
Kwa upande wa Mashirika, Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Plan International limejitolea kushirikiana na Serikali katika kuwasaidia vijana nchini kujiwezesha kiuchumi kwa kuratibu Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) ambao unawapa fursa vijana wanaoishi katika mazingira magumu kuchangamkia fursa za elimu ya ufundi zinazotolewa na Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA).
Mradi huo wa miaka mitatu unafanyika katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
Meneja wa Mradi huo, Bw. Simon Ndembeka anasema kuwa mradi una lengo la kuwasaidia vijana wapatao 9100 ambapo asilimia 53 wakiwa wakike kupata elimu ya ufundi katika fani mbalimbali ambapo nia na madhumuni ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa  na kuendesha maisha yao ili kupunguza kasi ya umasikini nchini.
“Mradi huu umelenga vijana wanaoishi katika mazingira magumu ambao wanatamani kujiendeleza kielimu lakini hawana uwezo huo hivyo tunawasihi vijana mchangamkie fursa iliyotolewa kupitia shirika letu ili muweze kuendeleza maisha yenu”, alisema Ndembeka.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Plan International-Tanzania, Bi. Gwynneth Wong amesema kuwa mradi umeokoa vijana wengi kutoka katika mazingira hatarishi na kuwafanya wawe na uwezo wa kujitegemea kwa kujishughulisha na biashara mbalimbali za halali.
Ameongeza kuwa asilimia 65 ya vijana 1225 waliohitimu mafunzo hayo wameajiriwa na wengine wamejiajiri hivyo inaonyesha dhahiri kuwa miradi hii ya kuwainua vijana kiuchumi inaleta mafanikio makubwa kwa vijana na taifa kiujumla.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa YEE Kanda ya Mashariki, Adolf Jeremiah amesema kuwa mradi huo hautoishia kuwapatia ujuzi tu bali utaendelea kuwawezesha kichumi ili kuhakikisha vijana hao wanasimama imara na wanapata maendeleo kupitia fani walizozisomea.
“Shirika la Plan International tumeamua kusaidia vijana kwa hali na mali hivyo ni lazima kuhakikisha wanayafikia malengo yao, kwa sasa tumewasiliana na VETA wafanye tathmini ya vifaa vinavyotakiwa na vijana hao ili tuweze kuvinunua na kuwagawia waendeleze fani zao zinazowasaidia katika maisha yao ya kila siku”, alisema Jeremiah.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA - Pwani, Joseph Deusdedit amesema kuwa kadri mradi unavyoendelea ndivyo wavyozidi kutoa nafasi nyingi za vijana kupata elimu ya ufundi katika chuo hicho pia wameendelea kuwatengea sehemu za kupata mafunzo zilizo karibu na maeneo wanayoishi kwa ajili ya kuwawezesha kutambua kiurahisi fursa zilizopo katika maeneo yanayowazunguka pia kuwapunguzia gharama za usafiri.
“Nitajitahidi kushauriana na wadau wengine kufanya elimu hii ya vijana wanaoishi kwenye mazingira magumu kuwa endelevu hata kama mradi hautoendelea kwa sababu mradi huo umeonyesha mafanikio na unalenga vijana wa aina zote wakiwemo walemavu, waliosoma na wasiosoma hivyo kuondoa adha kubwa ya utegemezi katika familia zao,” alisema Deusdedit.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Future World, Robert Mkolla amesema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ambao ndio asilimia kubwa ya watanzania ni janga kubwa kiuchumi na kiusalama kwani vitendo vingi viovu vinafanywa na vijana wasio na kazi za kuwaingizia vipato hivyo shirika la Plan limeokoa vijana wengi katika matatizo ya namna hiyo.
Mbali na kupewa mafunzo ya elimu ya ufundi, Shirika la Uhamasishaji Hifadhi Kisarawe (UHIKI) linatoa mafunzo ya kuweka na kukopa fedha kwa vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi chini ya mradi YEE ili kuwaelimisha jinsi ya kutunza fedha zao.
Afisa Msimamizi wa Miradi ya Kuweka na Kukopa – Kisarawe, Vuai Shame anasema kuwa kuna umuhimu wa vijana kupata elimu juu ya utunzaji wa fedha pamoja na upatikanaji wa mikopo ili waweze kuimarisha biashara zao na kuona faida inayopatikana kutokana na biashara hizo.
“Kazi ya UHIKI ni kuwasimamia vijana ili waweze kuunda vikundi vya kuweka na kukopa fedha zitakazowasaidia kuendeleza biashara zao, mpaka sasa tumefanikiwa kuwa na vikundi 27 vya vijana vilivyopo katika kata 4 za wilaya yetu lakini bado tunaendelea kuwahamasisha vijana wengine kufanya hivyo kwani vikundi vina faida”, alisema Shame.
Mradi huu unaendelea kuwasaidia vijana wengi na umeonesha manufaa makubwa kwa jamii kiasi kwamba Serikali inatambua mchango wao wa hali na mali.
Afisa Maendeleo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Yahaya Mbogolume anasema kuwa mradi huo umekuja wakati muafaka kwani umekuwa chachu ya maendeleo ya Halmashauri hiyo kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni vijana ambao walikuwa hawana cha kufanya lakini kupitia fursa hiyo vijana wameweza kujiajiri.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii – Kata ya Vingunguti, Pius Majura anasema kuwa, Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupunguza utegemezi kwa kuwasaidia vijana na wanawake kuweza kusimama wenyewe kwa kufanya shughuli zao mbalimbali hivyo, mradi huo umewasaidia vijana wa eneo hilo kuacha kufanya uhalifu na badala yake wamejikita katika shughuli za halali ambazo zinawasaidia kupata kipato cha kuwawezesha kuendesha maisha yao.
“Kabla ya mradi huu kuanza vijana wengi walikuwa wakijihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya na wasichana wengi walikua wakifanya biashara za kuuza miili yao, madanguro yalikuwa mengi lakini baada ya vijana kupatiwa elimu na wengine kuweza kujiajiri na kuajiriwa, uhalifu umepungua kwa asilimia kubwa”, alisema Majura.
Kwa upande wake mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya mradi huo, George Geligoali anatoa rai kwa vijana wenzie kuacha kudharau fursa zinazotolewa na makampuni mbalimbali na badala yake wazichangamkie kwa kuwa fursa hizo ni kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kiujumla.
Mhitimu mwingine Rajabu Kilanga anasema kuwa mradi huo umemuwezesha kufahamu jinsi ya kuhifadhi fedha kwa ajili ya maisha ya baadaye pia umemnufaisha yeye pamoja na familia yake kwani kupitia fani ya umeme aliyoisomea ameweza kupata tenda ndogo ndogo ambazo zinamsaidia kuyaendesha maisha yake.
“Pamoja na faida nyingi nilizozipata kupitia mradi huu lakini ukosefu wa ajira za kudumu ni moja ya changamoto ambazo zinatukabili vijana tuliohitimu mafunzo haya hivyo, tunaiomba Serikali itusaidie kutupatia ajira ili na sisi tuweze kutimiza malengo yetu na kuchangia katika kulijenga Taifa letu”, alisema Kilanga. 
Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) -Tanzania, pia unashughulika na kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupata Elimu ya ufundi kwani jamii bado haijatambua umuhimu wa kuwapatia elimu watu wenye ulemavu. 
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment