Image
Image

Serikali yawasilisha ukomo wa bajeti na mpango wa maendeleo wa miaka mitano Bungeni.

SERIKALI imewasilisha ukomo wa bajeti na mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaolenga kuiweka Tanzania katika safari kamili ya viwanda. 
Aidha serikali inatarajia kutumia kiasi cha Sh trilioni 32.476 kwa mwaka 2018/19 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.4 ya bajeti ya mwaka 2017/18 ambazo zilikuwa Sh trilioni 31.712.
Aidha, imetaja shabaha na malengo ya uchumi sita ambayo ni pamoja na kuhakikisha ukuaji wa Pato Halisi la Taifa, kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kukua kwa mapato ya kodi. Kati ya fedha hizo, Sh trilioni 22.088 sawa na asilimia 68 ya mahitaji yote, ni mapato ya ndani ambayo mapato ya kodi ni Sh trilioni 18.8 sawa na asilimia 85.2 ya mapato yote, mapato yasiyo ya kodi ni Sh tril 2.4.
Mapato ya halmashauri ni Sh bilioni 847.7 na hivyo ili kukamilisha bajeti serikali inahitaji Sh trilioni 10.388 ambazo ni mikopo kutoka ndani na nje ya nchi. Kiasi hicho cha fedha kilitajwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bungeni jana Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19.
Akitoa ufafanuzi kuhusu makisio ya bajeti hiyo ya mwaka 2018/19 ya Sh trilioni 32.476, Dk Mpango alisema kati yake Sh trilioni 20.227 zitakuwa za matumizi ya kawaida na Sh trilioni 12.248 ni za maendeleo.
Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Sh trilioni 7.627 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma, Sh trilioni 9.705 ni kwa ajili ya deni la taifa ambalo hadi Juni mwaka huu lilikua na kufikia dola za Marekani milioni 26,115.2 sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 22,320.76, katika kipindi hicho mwaka 2016.
Alisema kwa upande wa fedha za matumizi ya maendeleo, Sh trilioni 9.536 au asilimia 76.6 ni fedha za ndani na zinazobaki zitakopwa kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.
Aidha, Dk Mpango alitaja shabaha na malengo ya uchumi sita katika kipindi cha muda wa kati cha mwaka 2018/19 hadi mwaka 2020/21 kuwa ni kuhakikisha kwamba ukuaji wa pato la halisi ya Taifa unafikia asilimia 7.1 katika mwaka 2017.
“Pia shabaha na malengo ya uchumi yanalenga kudhibiti kasi ya mfumo wa bei kutoka wastani wa asilimia 5.3 ya mwezi Juni mwaka huu hadi asilimia 5.0 ifikapo Juni mwakani,” alisema.
Alisema mapato ya kodi kukua na kuwa asilimia 14.2 ya Pato la Taifa katika mwaka 2018/19 sawa na ilivyokuwa katika mwaka 2017/18. Dk Mpango alisema matumizi ya serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 24.5 ya Pato la Taifa katika mwaka 2018/19 ikilinganishwa na asilimia 26.2 mwaka 2017/18.“Kupunguza nakisi ya bajeti ikijumuishwa na misaada kutoka asilimia 3.8 mwaka 2017/18 hadi asilimia 2.5 mwaka 2018/19,” alisema Dk Mpango. Pia alisema kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Dk Mpango alisema misingi ya mpango na bajeti mitano katika kipindi hicho ni pamoja na kuendelea kuimarishwa na kudumishwa kwa amani, usalama, utulivu na umoja nchini na nchi jirani.“Kuimarisha kwa viashiria va uchumi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama vile Pato la Taifa, ukusanyaji wa mapato ya ndani na mfumuko wa bei,” alisema. Pia alisema ni kuendelea kuimarika na kutengemaa kwa uchumi wa dunia, kuendelea kuwa na utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia na kuwa na hali ya hewa nzuri ndani ya nchi katika nchi jirani.
Alisema mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2018/19 utakuwa wa tatu katika mwendelezo wa kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano. Alisema mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo yamezingatia Malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa ya Miaka mitano (2016/17-2020/21) hususani katika kuendeleza kasi ya ukuaji uchumi na kuimarisha kasi ya utekelezaji wa mpango hasa kwa kutatua changamoto za upatikanaji wa fedha na mitaji.“Pia yamezingatia upatikanaji wa ardhi na maeneo ya uwekezaji na kuimarisha mipango miji na maendeleo ya makazi, kuongeza uzalishaji wa bidhaa viwandani, kuongeza uwezo wa kupambana na umaskini na kuimarisha ustawi na maendeleo ya jamii kwa kutoa huduma bora afya, elimu, maji na kinga kwa jamii,” alisema.
Pia kuongeza matumizi ya teknolojia, ubunifu ujuzi na utoshelevu wa mahitaji ya rasilimali watu wenye weledi unaohitaji kwa ustawi wa uchumi wa viwanda na kuharakisha usalama wa chakula na majitaji ya lishe bora nchini.
Waziri Mpango alivataja vipaumbele na miradi itakayopewa msukumo wa kipekee katika mwaka 2018/19 ambayo itakuwa katika maeneo manne yanayohusu Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano.
Alisema miradi kielelezo ambayo utekelezaji wake utapewa msuko wa kipekee katika kujenga viwanda vya kukuza uchumi na hasa katika ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda ni pamoja na mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma, Kiwanda cha kufua chuma cha Liganga, shamba la miwa na kiwanda cha sukari Mkulazi, ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi kimiminika Lindi, uanzishwaji wa kanda maalumu za kiuchumi na kituo cha viwanda cha Kurasini.
Msukumo mwingine upo katika kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu eneo hili linalenga kuendeleza mafanikio ya ustawi wa maisha ya Watanzania hasa vijiji kwa kuboresha huduma za afya hasa za kibingwa, elimu na ujuzi huduma za ustawi wa jamii na upatikanaji wa uhakika wa chakula na lishe bora.
Dk Mpango alisema msukumo mwingine upo katika ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji eneo ambalo linalenga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, usafiri wa anga na usafiri wa majini.“Miradi itakayopewa msukumo ni pamoja na ujenzi wa bwawa na mitambo ya kufua umeme Stiegler’s Gorge, ujenzi wa reli ya kati na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania,” alisema Dk Mpango, alisema msukumo upo katika kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mipango ambako kunalenga ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa mpango, kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha kwa maandalizi ya utekelezaji wa miradi na kuweka vigezo vya upimaji mafanikio na utekelezaji.
“Serikali inaweza mkazo katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, miongoni mwa miradi hiyo ni wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam, kiwanda za kuzalisha dawa muhimu na vifaa tiba, na mradi wa Dar es Salaam-Chalinze na itaendelea kuongeza idadi ya miradi hiyo iliyo katika mfumo wa PPP,” alisema.
Dk Mpango alisema serikali imeweka mkakati wa kushirikisha sekta binafsi katima mwaka 2018/19, kwani sekta binafsi ndio mtekelezaji mkuu wa mpango kadiri ya dhana ya kujenga uchumi wa viswanda.“Serikali imeweka mikakati inayolenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mikakati ya kubainisha maeneo yatakayowezesha kuvutia wawekezaji wa sektsa binafsi na kuainisha vivuto kwa wawekezaji,” alisema.
Mpango alitoa maelekezo mahsusi katika uandaaji wa mipango na bajeti kwa mwaka 2018/19 kwa mujibu wa kifungu cha 17 (3) kanuni ya bajeti ya mwaka 2015, ambao inawataka maofisa masuhuli kuzingatia, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19 unalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu hali ya uchumi, utekelezaji wa bajeti na miradi ya maendeleo kwa mwaka uliopita na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kuvutia wawekezaji wa sekta binafsi katika viwanda na juhudi za kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ya kujenga uchumi wenye hadhi ya kipato cha kati.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment