Joseph Butiku Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Joseph Butiku amesema asingekubali kushiriki katika Tume hiyo laiti kama
angejua CCM ingeingilia mchakato huo.
Butiku ambaye alitoa kauli hizo kwa
nyakati tofauti, wikiendi iliyopita kwenye Mabaraza ya Katiba ya Halmashauri ya
Mji wa Soni, Lushoto na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, alieleza
kutokufurahishwa kwake na kitendo cha CCM kushinikiza maoni yake mbele ya
mabaraza hayo.
Alilalamika kuwa kitabu cha mwongozo wa
utoaji maoni kilichotolewa na CCM kinatumiwa vibaya kushinikiza maoni kwenye
Rasimu ya Katiba Mpya.
“CCM imeandaa kitabu kizuri kweli
kusaidia wanachama wake, tuliwaambia (Tume) hatukitaki; ni mwongozo kusaidia
wanachama wake namna ya kutoa maoni, lakini kimekuwa kinatumika vibaya.
Kinatumika kushinikiza maoni,” alisema Butiku.
Butiku ambaye ni mwanachama wa Tanu tangu
mwaka 1958 na CCM kuanzia 1977 alisema: “Ningejua itatokea chama kitafanya
hivyo, nisingekula kiapo nilichokula kufanya kazi hii katika Tume ya
Marekebisho ya Katiba. Kundi moja lisigeuke Tanzania. Mimi ni mzee nasema kitu
kikubwa nataka Mwenyekiti (wa CCM) asikie, Halmashauri Kuu yangu (ya CCM)
isikie. Mchakato huu usiingiliwe, madiwani saidieni wananchi wenu kujielewa.
Muungano hautaponywa kwa helikopta zinazoruka au vitabu vinavyosambazwa.”
Muungano
Kuhusu Muungano, Butiku aliyewahi kushika
nyadhifa mbalimbali serikalini alisema: “Mimi ni mzee sasa, sitaki kwenda
kaburini bila kuwaambia ukweli. Endeleeni kuujadili, msifanye jambo la kutaka
asali bila kujua madhara yake,” alisema.Kauli hiyo ya Butiku ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere ilitokana na wajumbe
kuonyesha mvutano kuhusu muundo wa Serikali katika Muungano na wengi
walionekana kuelemea upande wa Serikali mbili uliopo sasa, baadhi kuunga mkono
Rasimu ya Katiba inayopendekeza Serikali tatu, huku wachache wakitaka Serikali
moja.
Butiku aliwataka wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba kutoa maoni yanayolenga kulinda na siyo kuvunja Muungano na kwamba Tume
ya Marekebisho ya Katiba imepewa kazi ya kuulinda akisisitiza kwamba haikuwa,
wala haina ajenda ya kuvunja.
“Wapo pia viongozi wakubwa ndani ya
Baraza la Wawakilishi, wengine wamestaafu, hawautaki Muungano. Tume inawafahamu
wanaotaka Tume ya Katiba iwe na ajenda ya kuvunja Muungano. Muungano huu,
ulimfukuza Aboud Jumbe madarakani, kiongozi mkubwa tu, mi nawaambia mambo mengine
siri. Jumbe alitoka kwenye mkutano wa CCM, kaja pale nje akakuta gari lake
lingine siyo la Makamu. Leo, (anamtaja kiongozi huyo) anasema tulifanya makosa
kuungana, anajiunga na Jumbe, anaanza kufanana na Uamsho,” alisema Butiku.
Butiku aliifananisha Katiba Mpya nzuri
kuwa sawa na asali akieleza kuwa inahitaji umakini wakati wa kuiandaa,
akifafanua kuwa unapoandaa asali lazima uwe makini vinginevyo unaweza kuambulia
kushambuliwa na nyuki.
“Wajumbe
msipokuwa wa kweli, badala yake watu wakaumwa na nyuki, mtatulaumu. Ukweli
wanaufahamu wote ili waweze kuamua? Tumekubaliana kwenye Tume tuambiane ukweli
ili tupate asalisema.”
Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment