Joseph Butiku
Viongozi nchini wametahadharishwa kuacha kupokea
zawadi na kuzihalalisha kwa kuzipa jina la takrima.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku, alipokuwa akijibu swali la Mjumbe wa
Baraza la Mabadiliko ya Katiba wilayani Handeni, Zawadi Chamosi.
Chamozi alitaka kupewa ufafanuzi kuhusu maana ya
zawadi katika utumishi wa umma kwa mujibu wa ibara ya 15 kifungu kidogo cha
kwanza.
Butiku alisema kuwa kiongozi akikubali kupewa
zawadi anaweza hata kuuza siri za nchi kwani atalazimika kufuata matakwa ya
aliyempa zawadi hiyo kama kulipa fadhila.
Hata hivyo alisema kitendo hicho ni kinyume na
taratibu kwa mujibu wa sheria za kazi.
“Ningependa niwaambie kitu kimoja
katika kifungu hiki, unaweza kupewa zawadi kutoka kwa wananchi kutokana na
utendaji wako wa kazi, haikatazwi kwani kwa utaratibu kama ilivyoelezwa hapa
zawadi hiyo ni zawadi ya Jamhuri ya Muungano," alisema.
Aidha alitolea ufafanuzi kuhusu hoja iliyotolewa
na Diwani wa kata ya Kwamatuku, Mustafa Beleko, aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa
baraza hilo kuhusu ibara ya 16 kifungu cha kwanza, ibara ndogo ya kwanza
kifungu (b) kinachomtaka kiongozi wa umma kutangaza mali zake na za mwenzi wake
na kwamba itahusu wake wote wa ndoa wa mhusika wanaotambulika kisheria.
“Hata kama ana wake wangapi ili mradi
wanatambulika kisheria, atapaswa kutaja mali zao zote kwani wanashirikiana
katika shughuli zao za kila siku, ni lazima mali na madeni yake yafahamike ili
kujua idadi za mali zenu pamoja na watoto wenu wenye umri zaidi ya miaka kumi
na nane,” alisisitiza.


0 comments:
Post a Comment