Jaji Joseph Warioba.
Na. Mwandishi wetu kigoma.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepuuza
kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, ya kuwataka
wasikusanye maoni ya wananchi na kusema kuwa kitaendelea kufanya hivyo kwa kuwa
hakuna sheria wala kanuni iliyokiukwa na chama hicho.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya mpya Kakonko
Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, John
Mnyika, alisema kauli ya Warioba inakinzana na muongozo wa mabaraza ya asasi
ambao yeye mwenyewe aliusaini.
"Kauli ya Warioba ina mwelekeo wa kukiuka
kifungu cha 18(6) cha Sheria ya Katiba, ambacho kinatamka bayana kwamba, asasi,
watu wenye malengo yanayofanana na taasisi, kama Chadema zinaweza
kukusanya maoni ya wanachama wao.
Chadema inaendesha mabaraza yake ya katiba kwa
mujibu wa sheria.
Chadema iliandika barua Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Julai 8, mwaka huu na 10 Julai, Tume ilijibu kuitambua Chadema kuwa
taasisi yenye kuweza kukusanya maoni,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa chama hicho kina wanachama wengi
nchi nzima na muongozo wa kuhusu mabaraza ya asasi, taasisi na makundi ya watu
wenye malengo yanayofanana uliotolewa na Tume na kusainiwa na yeye mwenyewe
Warioba kama Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema mwongozo huo umeruhusu asasi, taasisi na
makundi ya watu wenye malengo yanayofanana ambazo zina mfumo wa kiuendeshaji
kuanzia ngazi ya chini hadi taifa, kukusanya maoni kuanzia ngazi hizo na
kuyawasilisha tume, kupitia ngazi ya taifa.
"Warioba ametoa kauli hiyo baada ya Chadema
kukutana na wanachama na wapenzi wake na kuonekana kuna wananchi wengi ambao
hawakufikiwa na Tume kutoa maoni yao," alisema.
Mpaka sasa chama hicho kimefanya mikutano ya
Mabaraza ya Katiba katika mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera,
Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga na Singida.
"Mikutano hiyo tunaifanya kwa kufuata
taratibu halali za kisheria. Hivyo kauli ya Warioba imekiuka hata mwongozo
aliousaini yeye mwenyewe, Chadema tunavyofanya...kukusanya maoni ya wanachama
wetu ili hatimaye tuyawasilishe.
Sisi tunaendeshwa na falsafa ya nguvu ya umma,
tuna umma mkubwa nyuma yetu, hatuwezi kukutana kwenye ukumbi pekee kama
wanavyofanya CCM na taasisi nyingine.
Tumeweka utaratibu wa kufanya mikutano na
mikusanyiko, kupitia Rasimu ya Katiba Mpya, watu kukusanya maoni juu ya rasimu
hiyo," alisema Mnyika.
Hivi karibuni, Jaji Warioba wakati akifunga
mjadala wa siku mbili wa Rasimu ya Katiba, uliofanywa na Baraza la Katiba la
Wabunge Wanawake, alikemea vyama vya siasa kupenyeza maoni yao katika Mabaraza
ya Katiba.
“Nazungumza wazi hapa leo, vyama vya siasa ni
taasisi, vifuate utaratibu vijadili kama Baraza la katiba la Taasisi na
kutuwasilishia maoni yao, sisi Tume hatutachukua maoni ya jukwaani wala ya
kwenye helikopta," alikaririwa Jaji Warioba akisema.
“Ukiangalia kwenye Katiba hii, utaona kuwa
wananchi wanataka dira ya Taifa, dira ya uchumi, kisiasa na kijamii, lakini cha
kushangaza mambo yanayozungumzwa ni machache tu ya madaraka, sasa haya mengine
yataboreshwaje?,''alihoji.
Alitaka wanasiasa wasitafute mchawi katika
mvutano na mjadala unaoendelea wa kipengele cha Rasimu ya Katiba
kinachopendekeza serikali tatu, kwa kuwa kimetokana na maoni ya wananchi na si
ya Tume.




0 comments:
Post a Comment