kurugenzi wa
Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe.
Kile kitendawili cha siku nyingi lini
kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani kitaanza kujengwa katika eneo
la Mbezi Luis kimeteguliwa baada ya Jiji kueleza kuwa ifkikapo Novemba mwaka
huu kituo hicho kitaanza kujengwa.
Mwezi Januari mwaka huu, Halmashauri ya Jiji la
Dar es Salaam ilibomoa majengo yote yaliyokuwamo katika kituo cha Ubungo na
kubakiza jengo moja la utawala, ikiwa ni maandalizi ya kuachia eneo hilo kwa
ajili ya kujenga kituo cha mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (Dart).
Baada ya Jiji kubomoa kituo hicho, lilikaa
kimya bila kusema nini kinachoendelea huku likiahidi kwamba, kituo hicho
kinachotumiwa na mabasi yaendayo mikoani kingehamishiwa Mbezi Luis.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa
Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, alisema kuwa ujenzi wa kituo cha Mabasi
yaendayo mikoani katika eneo la Mbezi Luis unatarajia kuanza Novemba mwaka huu
baada ya kukamilika kwa taratibu mbalimbali.
Alisema kwa sasa mchakato wa kumtafuta
mkandarasi atakayejenga kituo hicho unafanyika, na unatarajiwa kukamilika ndani
ya miezi miwili kuanzia sasa.
Kabwe alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho pindi
utakapokamilika kitakuwa kituo kikubwa na cha kimataifa tofauti na kile cha
awali cha eneo la Ubungo.
Aliongeza kuwa kituo hicho kitakuwa ni cha
kudumu kwa kipindi kirefu kutoka kizazi hadi kizazi na hakitakuwa kituo cha
muda au cha kuhama kwa miaka ya karibuni.
“Kitakuwa ni kituo kikubwa, unapozungumzia kituo
cha mabasi yaendayo mikoani siyo kitu cha mchezo lazima tujipange kwelikweli
kwa ujenzi, na hicho kituo kitakuwa ni cha miaka 70 ijayo,” alisema Kabwe.
Alisema kinachochelewesha kujengwa kwa kituo
hicho kwa muda mrefu ni upatikanaji wa mkandarasi mwenye sifa na vigezo vya
kujenga kituo, na kusema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam haikurupuki
katika kutafuta mkandarasi, hivyo lazima utaratibu ufuatwe.
Kabwe alisema kuwa kwa sasa timu yake ya Jiji
iko na washauri wataalam kwa ajili ya kuweka michoro ya ramani ya ujenzi wa
kituo cha kisasa kitakacho chukua magari mengi.
Eneo la kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo awali
ilikuwa eneo la Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kabla Serikali
kubadilisha matumizi yake na kuwa kituo cha mabasi ya kwenda mikoani na nchi
jirani.
Hata hivyo serikali hiyo hiyo imebadilisha matumizi ya
kituo cha mabasi ya mikoani na kuwa kituo cha magari ya mwendo kasi DART mradi
unaotarajia kukamilika mwaka 2014.
DART WAZUNGUMZIA UJENZI WA KITUO NA KARAKANA
ENEO LA UBUNGO
Kwa upande wake, mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart)
walipotafutwa ili kueleza ni lini ujenzi wa kituo na karakana utaanza kujengwa
baada ya wafanyabiashara wote kuondolewa, mtaalamu mshauri mawasiliano wa Dart,
Jack Meena alisema kazi ya ujenzi ilishindikana kuanza mapema kutokana na
kukosekana kwa fedha za kulipia fidia kwa waathirika wa ujenzi.
Alisema sababu nyingine ni katika kipindi
ambacho mkandandarasi alitakiwa aanze ujenzi kulitokea mafuriko ambayo yalizuia
kuanza kwa ujenzi ( Mvua zilizonyesha mwaka 2011).
Sababu nyingine Meena alisema ni kufunguliwa
kwa kesi mahakamani na wafidiwa.
Kutokana na kesi hizo kulikuwa na zuio la
mahakama kusitisha ujenzi mpaka kesi zitakapomalizika
Hata hivyo, alisema
Serikali ipokatika mchakato wa kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa
vituo vya mabasi yaendayo mikoani kupitia sera ya Public Private Partnership
(PPP), na kusema kuwa kwa sasa bado mabasi hayo yataendelea kufanya shughuli
zake katika kituo cha Ubungo mpaka hapo miundombinu itakapojengwa na
kukamilika.
TANROADS WAZUNGUMZIA UJENZI WA VITUO VYA DALADALA
Wakala
wa Barabara Tanzania (Tanroads) walipoulizwa ujenzi wa vituo vya daladala kwa
ajili ya mabasi ya Dart utakamilika lini, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi
Patrick Mfugale alijibu kuwa miundombinu na vituo vinatarajiwa kukamilika
Machi, 2015 endapo hapatakuwa na ucheleweshwaji wowote katika utekelezaji wa
mikataba ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
Alipoulizwa sababu gani zinazosababisha kutoanza
kujengwa kwa karakana ya mabasi ya mradi wa Dart katika eneo la Ubungo wakati
ubomoaji wa vibanda vilivyokuwapo katika eneo hilo ulifanyika muda mrefu.
Aliongeza kwa kusema kuwa Tanroads inaendelea
kufanya mazungumzo na wadau kupitia na kuridhia mapitio ya usanifu ujenzi
utaanza mara moja.
“Awali ujenzi wa karakana ulitarajiwa kukamilika
ndani ya miaka miwili, lakini kutokana na kupungua kwa kazi baada ya kuhamishwa
kwa kituo cha mabasi yaendayo mkoani, ujenzi utachukua kati muda wa mwaka mmoja
hadi mwaka mmoja na nusu,” alisema Mfugale



0 comments:
Post a Comment