WAZIRI MKUU
Mhe. Mizengo Pinda anaondoka Dar es Salaam leo kwenda China kwa ziara ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya
nchi hiyo inayotarajiwa kuanza kesho, Oktoba 16.
Kwa mujibu
wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni kutangaza fursa za uwekezaji hapa nchini,
fursa za biashara, utalii na kutafuta mitaji kwa ajili ya sekta zilizo chini
mpango wa matokeo makubwa ya haraka (Big Results Now Initiative).
Akiwa China,
Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Li Keqiang
na viongozi wa Serikali ya China katika sekta za uchukuzi, mawasiliano,
viwanda, madini na nishati.
Pinda atatembelea
mji wa Beijing na majimbo ya Shenzen, Chengdu na Guangzhou ambako atakutana na
Makamu wa Rais wa China, Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya
Maendeleo ya China, wakuu wa mashirika makubwa na kampuni kubwa nchini China na
kufanya nao mazungumzo.
Waziri Mkuu
Pinda ataungana na Wakuu wa Nchi watano kwenye ufunguzi wa maonyesho ya
kibiashara ya magharibi mwa China (Western China International Fair – WCIF)
ambako atahutubia washiriki wa maonyesho hayo.
Pia atatembelea maeneo kadhaa ya
uwekezaji na kufungua Kongamano la Uwekezaji baina ya Tanzania na China
litakalofanyika Guangzhou.
Vilevile, Waziri Mkuu anatarajiwa kufungua mafunzo ya
siku 10 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali za hapa nchini
yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya
Uongozi ya Tanzania.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha
utendaji wa Maeneo ya Uzalishaji kwa
Mauzo ya Nje (EPZ).
Waziri Mkuu
ambaye anafuatana na Mawaziri wanne, wabunge wawili, wakuu wa mikoa watatu,
wakuu wa taasisi wa Serikali na wawakilishi kutoka sekta binafsi, anatarajiwa
kukutana na Watanzania waishia China huko Beijing na Guangzhou.
Tanzania
imekuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na China, nchi kubwa ya Bara la
Asia, tangu mwaka 1964.
China yenye
ukubwa wa kilometa za mraba 9,596,961 ina wakazi wapatao 1,349,585,838.
Kwa
mujibu wa takwimu za Shirika Fedha la Kimataifa (IMF) nchi hiyo ni ya pili kwa
uchumi mkubwa duniani.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S. L. P.
3021,
DAR ES
SALAAM.
JUMANNE, OKTOBA 15, 2013


0 comments:
Post a Comment