Image
Image

JK: Fimbo ya kutunyima misaada haifai.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kamwe mahusiano kati ya Tanzania na wabia wa maendeleo hayawezi kutawaliwa na vitisho vya wabia hao wa maendeleo kuikatia Tanzania misaada kwa sababu yoyote ile.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kamwe Serikali yake haiwezi kukubali kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima na vitisho hivyo na ikifika mahali Serikali itawaambia wabia hao kubakia na misaada yao.

Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Serikali yake wakati alipozungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership - OGP) Kanda ya Afrika ulioanza , Jumatano, Mei 20, mwaka 2015, katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Rais Kikwete alielezea, kwa undani, hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa na Serikali yake kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi na hatua za kupanua uhuru na uwazi katika taasisi mbali mbali za Kiserikali na binafsi.

Aidha, Rais Kikwete amezungumzia upinzani ambao umekuwa unajitokeza kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao (Cyber Crime) na kusema kuwa njia bora zaidi ya kufikia mwafaka siyo kwa kila upande kutoa vitisho ama lawama kwa mwenzake bali ni kwa pande zote mbili kukaa chini na kujadili namna gani ya kuboresha Sheria hiyo kama kweli Sheria hiyo inayo hitilafu zinazodaiwa na baadhi ya taasisi zisizokuwa za Kiserikali na baadhi ya vyombo vya habari.

“Tukikaa pamoja yataisha kwa urahisi. Na tayari Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia amekaribisha maoni na mawazo kuhusu jinsi ya kuboresha Sheria hiyo. Nyie mmepeleka maoni yenu?” ameuliza Rais Kikwete bila kupata jibu kutoka kwa washiriki ambao ni pamoja na taasisi zisizokuwa za kiserikali.

“Wengine wao wameanza kuingilia na kusema kuwa wasipobadilisha Sheria hiyo basi hawatatoa misaada kwa Tanzania. Msimamo huu hausaidii na unaweza kuwa na matokeo hasi (counter-productive). Mkitufikisha hapo, sisi Serikali yetu itakataa…lakini ubabe huu hausaidii. Unajua Serikali nayo inahitaji heshima yake…ukitaka kuonyesha ubabe nayo itaonyesha ubabe pia,” Rais Kikwete amewaambia washiriki wa Mkutano huo ambao ni pamoja na wawakilishi wa wabia wa maendeleo wa Tanzania.

Ameongeza: “Ukiitishia Serikali kuwa isipofanya hivi hatuipi misaada, na sisi tutafika mahali tutawambia kaeni na misaada yenu na sisi tukae na heshima yetu. Kamwe haiwezekani wale tunaoshirikiana nao katika maendeleo wakatumia fimbo yao kushinikiza kuwa usipofanya hivi wanakatalia misaada. Tutafika mahali tutasema kuwa mnatudhalilisha mno…tutasema kuwa hapa mlipotufikisha panatosha…kaeni na misaada yenu. Tutaona namna gani ya kujiendesha wenyewe,” amesema Rais Kikwete.

Amesisititiza: “Vitisho havijengi. Tutafute fursa ya mazungumzo kwa sababu ni fursa hiyo inayotoa majawabu ya changamoto zote.”

Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa na nchi zote nane za Afrika ambazo ni wanachama wa OGP kati ya nchi 65 duniani ambazo zimejiunga na utekelezaji wa dhana ya uwazi OGP. Nchi za Afrika ni Afrika Kusini iliyokuwa ya kwanza katika Afrika kujiunga ikifuatiwa na Tanzania. Nchi nyingine za Afrika wanachama wa OGP ni Malawi, Ghana, Kenya, Liberia, Sierra Leone na Tunisia.

Nchi nyingine za Afrika ambazo zinashiriki Mkutano huo wa OGP hata kama siyo wanachama wa OGP iliyoanzishwa Septemba 2011 mjini New York, Marekani ni Botswana, Nigeria, Zambia, Uganda, Zimbabwe na IvoryCoast.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amewasili mjini Dodoma tayari kwa vikao mbali mbali vya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ndiye Mwenyekiti wake.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

20 Mei, 2015
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment