Image
Image

Stars kwenda Uganda keshokutwa.

Kikosi cha timu ya taifa ya soka (Taifa Stars) kinatarajia kuondoka nchini keshokutwa, kuelekea jijini Kampala kwa ajili ya mechi ya marudiano ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Nyumbani (CHAN) 2016 dhidi ya wenyeji Uganda utakaopigwa kwenye Uwanja wa Nakivubo, Jumamosi.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa, alisema kwamba mazoezi ya kikosi hicho yanaendelea vyema.
Alisema kwamba wachezaji watakaosafiri kuelekea Kampala Alhamisi watajulikana baada ya mazoezi ya mwisho kesho jioni na yatatokana na ripoti ya daktari wa timu hiyo.
"Najua kila mmoja anahitaji kuona tunavuna matokeo mazuri, wachezaji wanajua na sisi makocha tunajua kiu waliyonayo mashabiki," alisema kocha huyo ambaye bado pia anaifundisha Yanga kama kocha msaidizi.
Kikosi cha Stars kimeweka kambi yake mjini Bagamoyo, mkoani Pwani na kinafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterani huku benchi la ufundi likiruhusu mashabiki kuangalia mazoezi hayo.
Alisema lengo la kuwaweka nje ya mji ni kuwapa muda wa kupumzika na kufikiria mazoezi tu.
Wachezaji walioitwa katika kikosi cha Stars na wanaendelea na mazoezi ni pamoja na Mwadini Ally wa Azam, Ally Mustapha  'Barthez' (Yanga), Mudathir Khamis (KMKM), Shomari Kapombe (Azam), Michael Haidan (Ruvu Shooting), Mohammed Hussein (Simba), Mwinyi Hajj (KMKM), Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Abdi Banda (Simba) na Simon Msuva wa Yanga.
Wachezaji wengine ni Said Ndemla, Ramadhan Singano 'Messi' (Simba), Salum Telela (Yanga), Frank Domayo (Azam), Atupele Green (Kagera Sugar), Rashid Mandawa (Mwadui), Ame All (Azam), Deus Kaseke (Yanga),  Vicent Andrew (Mtibwa Sugar) na Mudathir Yahya wa Azam.
CANNAVARO NJIA PANDA
Nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro', ameliambia gazeti hili jana jioni kwamba anatarajia kuanza mazoezi mepesi leo jioni na hatima yake ya kusafiri kuelekea Kampala haijajulikana.
Beki huyo wa kati na nahodha wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara alisema kuwa mahali alipochanika (juu ya jicho), kidonda kinaendelea vizuri kutokana na madaktari wake kumshona 'kisasa'.
"Kidonda kinaendelea vizuri, siku hizi madaktari wanashona vizuri, ila kesho (leo) ndiyo nitaanza mazoezi mepesi na daktari ndiye atasema kama ninaweza kucheza Jumamosi," aliongeza Cannavaro.
Alisema eneo lililochanika ni palepale alipoumia katika mechi iliyopita dhidi ya watani zao, Simba na ameshonwa nyuzi tano.
Cranes itashuka uwanjani Jumamosi kurudiana na Stars ikiwa imeshatanguliza mguu mmoja katika fainali hizo za CHAN baada ya kuisambaratisha Stars kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar Juni 20, mwaka.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment