Magufuli aliteuliwa baada ya kuvuka kizingiti cha kwanza na kutinga
tano bora akiwa sambamba na Dk. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Balozi Amina
Salum Ali, Bernard Kamillius Membe na January Yusuf Makamba.
Baada ya mchujo huo nyota ya Magufuli iliendelea kung'ara baada ya
kutinga tatu bora na kuwapiku kwa kishindo Dk. Migiro na Balozi Amina,
hivyo kuwa mteule wa kuipeperusha bendera ya CCM hapo Oktoba 25, mwaka
huu.
Magufuli ambaye alichukua fomu rasmi Juni 5, mwaka huu, ni miongoni
mwa baadhi ya wagombea waliochukua fomu kimyakimya tofauti na wagombea
wengine maarufu waliochukua kwa mbwembwe kubwa huku wakizindua na
kutangaza nia zao kwa ahadi kibao.
Kuchukua fomu huko kimyakimya huku pia akizunguka kutafuta
wadhamini kwa staili hiyo, kunawafanya watu wengi kushindwa kujua
kipaumbele chake katika utendaji kazi wake endapo atafanikwa kushinda
katika uchaguzi mkuu Oktoba 25.
Awali kwa upande wa soka, wagombea wengi walitoa ahadi ya
kuhakikisha Tanzania inapiga hatua na kuepuka kuendelea kugeuzwa 'kichwa
cha wendawazimu' kwa kufungwa mara kwa mara na kushindwa kufuzu
michuano mikubwa ya kimataifa.
Tunakumbuka vema moja ya ahadi kubwa aliyoitoa na kuitekeleza Rais
wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, wakati wa harakati zake za
kuusaka urais kwamba ilikuwa ni kujenga uwanja mpya wa Taifa wa kisasa.
Mkapa alitangaza kipaumbele chake hicho kwa wadau wa michezo na
akahakikisha anasimamia mchakato huo na hatimaye kufanikisha zoezi hilo
na sasa Tanzania tunajivunia kuwa na uwanja bora kabisa wa michezo huku
pia ule wa zamani ukiendelea kukarabatiwa kwa kiwango cha kimataifa.
Pamoja na mambo mengine mengi aliyoyafanya Mkapa, lakini kwa upande
wa wadau wa michezo Tambarare Halisi ikiwa namba moja, hatuna budi kumshukuru na
kuendelea kumuombea maisha marefu kwa ahadi hiyo iliyotekelezeka.
Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, katika mchakato wake
wa kusaka urais 2005, kipaumbe chake kwa wanamichezo, aliahidi endapo
atafanikiwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali yake
itahakikisha timu za Taifa, zinapata makocha kutoka nje na itawalipa
mishahara katika kipindi chote.
Kikwete alikamilisha mchakato huo kwa Taifa Stars kuanza kunolewa
na makocha kutoka Brazil kabla ya baadaye kuwa chini ya Wadenmark na
sasa wazawa huku pia ngumi na netiboli zikiletewa makocha kwa nyakati
tofauti.
Kwa hilo pia, wadau wa michezo tutaendelea kumkumbuka Kikwete kwa
ahadi yake iliyotekelezeka, hivyo imani yetu na matarajio ni kusikia
anayempokea kijiti, Magufuli nini ambacho atatuahidi wadau wa michezo na
kukitekeleza kwa vitendo.
CCM imemtangaza Magufuli kuwa mgombea wake katika nafasi hiyo ikiwa
ni siku nne baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) katika
viwango vyake vya kila mwezi, kutangaza kuwa Tanzania ni ya 139 baada ya
kuporomoka kwa nafasi 12 kutoka mwezi uliopita, nafasi ambayo inaifanya
iburuze mkia kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Tambarare Halisi ikiwa mdau namba moja katika sekta ya michezo, linasubiri
sasa kusikia Magufuli akivunja ukimya wake na kutangaza endapo
atachaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Tanzania, ataisaidia vipi nchi yetu
kuweza kujulikana kimataifa kupitia michezo na hususan mchezo wa soka
ambao unaongoza duniani kwa kuwa na mashabiki wengi.
Tunatambua wazi kunahitajika mkakati wa dhati wa kiuwekezaji katika
soka la vijana ili kuhakikisha tunaondokana na kuitwa kichwa cha
wendawazimu na hilo linahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya wadau wa
soka, vyama vya soka, klabu na serikali.
Hivyo,Tambarare Halisi tunatarajia kusikia Magufuli naye akitueleza endapo
atafanikiwa kuiongoza Tanzania, mbali na ilani ya uchaguzi ya CCM,
kipaumbele chake kitakuwa nini katika kuisaidia sekta hii ambayo ni
chanzo kikubwa cha mapato na ajira kwa vijana.
Tunatambua ndani ya wiki mbili hizi, vyama vya upinzani navyo
vitatangaza wagombea wao katika nafasi hiyo, hivyo wadau wa michezo
wanasubiri ili kuweza kupima vipaumbele vyao hatua itakayowafanya
wasijutie uamuzi wao wa kura baadaye Oktoba 25, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment