Awali, uongozi wa klabu hiyo yenye makao makuu mtaa wa Msimbazi,
Kariakoo ulipanga kuipeleka timu Oman kwa ajili ya kuendelea na mazoezi
na pia kucheza mechi nyingine za kirafiki za kimataifa na timu za huko.
Akizungumza na gazeti hili jana, kocha wa Simba, Muingereza, Dylan
Kerr, alisema ameikataa kambi ya Oman kwa vile huko kuna hali ya hewa ya
joto kali na anaamini akiipeleka timu huko haitawajenga wachezaji wake.
Kerr alisema kwamba kuipeleka timu yake Oman kwa sasa ni sawa na
kuumiza wachezaji kutokana na mazoezi waliyofanya awali kabla ya kucheza
mechi ya Simba Day ambayo walishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na
kiungo, Awadh Juma.
"Oman kuna joto sana, kama hatutaenda Zanzibar, napendelea kikosi
changu kirejee Lushoto, ni sehemu nzuri ambayo ilisaidia kujenga stamina
ya wachezaji na tofauti ilionekana katika michezo iliyocheza, nataka
kiwango cha kila mchezaji kiimarike zaidi, najua ligi ni ngumu na ina
ushindani," alisema Kerr.
Aliongeza kwamba kipindi kilichobakia anahitaji kuwapa mbinu zaidi wachezaji baada ya stamina kuimarika.
Tangu kuwasili kwa kocha huyo, Simba imecheza mechi saba za kirafiki na imeshinda zote na kati ya hizo, mbili ni za kimataifa.
Simba imepangwa kuanza msimu mpya wa Ligi ya Bara ugenini
Mkwakwani, Tanga Septemba 16 mwaka huu dhidi ya African Sports
iliyopanda daraja kabla ya kuwavaa Mgambo Shooting kwenye uwanja huo
huo.


0 comments:
Post a Comment