Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limemtangaza refa, Israel Nkongo wa jijini Dar es Salaam kuwa ndiye atakayechezesha mechi ya Ngao ya Jamii itakayowakutanisha mabingwa wa msimu uliopita,Yanga dhidi ya Azam, Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.
Nkongo ndiye mwamuzi ambaye Yanga wamekosa bahati naye kwani ndiye
aliyechezesha mechi waliyopigwa 5-0 dhidi ya Simba Mei 6, 2012 na pia
waliyolala 3-1 dhidi ya Azam Machi 11, mwaka huohuo, ambayo wachezaji wa
mabingwa hao walimpiga na kukumbana na adhabu za vifungo.
Katika mechi hiyo dhidi ya Azam pia, kiungo Haruna Niyonzima na
nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' walitolewa kwa kadi nyekundu, huku
Stephano Mwasyika akikumbana na adhabu ya kufungiwa mwaka mzima kwa
kumpiga ngumi Nkongo uwanjani wakati wa vurugu za wachezaji wa Yanga
dhidi ya mwamuzi huyo.
Nkongo na wasaidizi wake walitoka siku hiyo kwa kusindikizwa na
askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) baada ya kupuliza kipenga cha
mwisho kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam.
Katika mechi ya keshokutwa, Nkongo atasaidiwa na Samuel Mpenzu
kutoka jijini Arusha, Josephat Daud Bulali (Tanga) na mwamuzi wa akiba
atakuwa ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamisaa wa mchezo huo
atakuwa Deogratius Rwechungura kutoka mkoani Mara.
Akizungumza jana jijini, Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Baraka
Kizuguto, alisema kuwa mechi hiyo itaanza saa 10:00 jioni na endapo
hatapatikana mshindi ndani ya dakika 90, hatua ya penalti itafuata.
Kizuguto alitaja kiingilio cha chini katika mchezo huo kuwa ni
Sh.7,000 kwa eneo la viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya
machungwa wakati VIP B na C mashabiki watalipia Sh.20,000.
Alisema kuwa tiketi zitauzwa siku ya mchezo na mashabiki watakata tiketi za VIP A watalipia Sh 30,000 kila mmoja.


0 comments:
Post a Comment