KUSHINDWA kuwepo kambini kwa wachezaji wa Yanga na Azam FC kumeharibu
ratiba ya maandalizi ya timu ya taifa, Taifa Stars, inayojiandaa kwa
mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Nigeria.
Taifa Stars itaikaribisha Nigeria, Super Eagles katika mchezo wa
kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika Gabon 2017, huku Tanzania
ikipangwa Kundi G pamoja na Nigeria, Misri na Chad.
Tayari Stars imeshafungwa 3-0 na Misri katika mchezo wa kwanza
uliofanyika mjini Alexandria na kushika mkia katika kundi lake
ikifuatiwa na Chad, ambayo nayo haina pointi lakini ilifungwa mabao 2-0
na Nigeria, ambayo ni machache ukilinganisha na Stars. Misri inayoongoza
kundi hilo kwa kuwa na pointi tatu sawa na Nigeria, iko juu kwa kuwa na
idadi kubwa ya mabao.
Akizungumza jana, Kocha Mkuu wa muda wa timu hiyo, Charles Mkwasa
alisema ratiba yake ya maandalizi imetibuka baada ya wachezaji wa Yanga
na Azam FC kuzuiwa kujiunga na timu hiyo.
Alisema wachezaji hao watajiunga na timu hiyo baada ya mchezo wa Ngao
ya Jamii utakaozikutanisha timu hizo Jumamosi Agosti 22 kwenye Uwanja
wa Taifa na kuondoka usiku kwenda Muscat, Oman, ambako Jumatatu
watacheza mchezo wa kirafiki.
Mkwasa alisema wachezaji hao watafanya mazoezi siku moja tu, muda
ambao hautoshi na yote hiyo imechangiwa na Yanga na Azam FC kutokuwa
tayari kuwaachia wachezaji wake kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii.
Taifa Stars imepata mwaliko wa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya
Taifa ya Oman Agosti 24 usiku, ambapo baada ya mchezo huo timu hiyo
itasafiri kwenda Uturuki jijini Istanbul.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Oman (OFA) liliomba kuche za
mchezo wa kirafiki na Taifa Stars kabla ya kuwavaa Turkemebistan katika
mchezo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia Septemba 03 kwa bara la
Asia, ambapo kocha wake mkuu Mfaransa Paul Leguen aliomba kucheza na
Stars.
Mara baada ya mchezo huo, Taifa Stars itakwenda Istanbul kwa kambi ya
wiki moja, ikiwa nchini Uturuki, Stars inatarajiwa kucheza michezo
miwili ya kirafiki kabla ya kurejea nchini kucheza na Nigeria Septemba
05.
Imeelezwa kuwa Mkwasa mwishoni mwa wiki atatangaza kikosi cha
wachezaji 22 watakaosafiri kwenda Uturuki kwa kambi hiyo. Aidha,
mshambuliaji Adi Yussuf anayechezea klabu ya Mansfield Towny ya
Uingereza alitarajiwa kujiunga na Stars nchini Uturuki, hatajiunga tena
kwa sababu ya maumivu.
Adi aliumia wiki iliyopita katika mchezo dhidi ya Nottingham Forest,
ambapo kwa sasa anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa klabu hiyo,
na pindi atapokuwa fit atapata nafasi ya kujumuika na kuitumika timu ya
Taifa ya Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment