Aliyekuwa mgombea wa kiti cha ubunge katika jimbo la
Lulindi kupitia CCM, Jerome Bwanausi ametangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho
baada ya kuwabwaga wenza watatu kutoka vyama vya NLD, CUF na ACT Wazalendo,
katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana.
Jerome ameshinda kiti hicho kwa kupata kura 17,715
sawa na asilimia 87.3, akifuatiwa na Modesta Makaidi wa chama cha NLD aliyepata
kura 1,638, Amina Mshamu wa CUF akipata kura 714 na mgombea wa ACT Wazalendo
Francis Ngaweje akiambulia kura 213.
Katika uchaguzi huo, idadi ndogo ya watu imejitokeza
kupiga kura ambapo kati ya watu 59,027 walioandikishwa ni watu 20,580 pekee
waliojitokeza sawa na asilimia 30.
Hali imekuwa tofauti na siku ya uchaguzi mkuu wa
Rais na madiwani Oktoba 25 ambapo katika jimbo hilo watu zaidi ya 45,000
walijitokeza kupiga kura.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana kuhusu
sababu za watu kutojitokeza kwa wingi, baadhi ya wakazi wa jimbo hilo lililoko
wilayani Masasi walidai kutokuwa na taarifa za tarehe ya kupiga kura huku
wengine hususani vijana wakidai kususia zoezi hilo kutokana na kukatishwa tama na
matokeo ya uchaguzi mkuu.
Idadi kubwa ya watu waliojitokeza ni watu wazima
wanaokadiriwa kuwa na umri wa kuanzia miaka 55 na kuendelea.
Uchaguzi huu mdogo umefanyika kufuatia kuahirishwa
hapo awali kutokana na makosa yaliyokuwa katika karatasi za kupigia kura ambapo
jina la mgombea wa CUF lilikosewa.
Kwa matokeo hayo, CCM imefanikiwa kuongeza kiti cha
ubunge wa majimbo katika bunge la 11 kutoka viti 188 hadi viti 189.


0 comments:
Post a Comment