Chama cha upinzani Myanmar cha National League for Democracy-NLD
kimeshinda viti vya kutosha bungeni kukiwezesha kumchagua Rais na kuunda
serikali ijayo.
Tume ya uchaguzi ya Myanmar imetangaza hii leo kuwa chama hicho cha
upinzani kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kimeshinda viti vingine
zaidi katika mabunge yote mawili nchini humo katika uchaguzi mkuu
uliofanyika Jumapili iliyopita na hivyo kupitisha idadi ya viti 329
vinavyohitajika kukiwezesha kumchagua Rais.
Ushindi huo mkubwa wa NLD unamaanisha kuwa chama hicho kinaweza kuwateua
wawili kati ya wagombea watatu wa wadhifa wa rais licha ya kuwa Suu Kyi
mwenye umri wa miaka 70 anazuiwa na katiba ya nchi hiyo kuwa Rais kwa
sababu wanawe wana uraia wa kigeni.
Chama hicho cha upinzani kinachosimamia misingi ya demokrasia kinayo
fursa ya kuuondoa utawala unaoungwa mkono na jeshi la Myanmar na kuipa
nafasi demokrasia na mageuzi ya kiuchumi.
Ukurasa mpya Myanmar
Baada ya zaidi ya miongo mitano ya utawala wa kijeshi nchini Myanmar,
Suu Kyi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ambaye leo anatimiza miaka
mitano tangu kuachiwa na jeshi kutoka kifungo cha nyumbani anatarajiwa
kuibadilisha sura ya kisiasa kwa kuwa na usemi mkubwa katika serikali
ijayo.
Lakini wachambuzi wanasema ushindi wa NLD sio mwisho wa ushawishi wa
jeshi la Myanmar kwani katiba inalihakikishia robo ya viti bungeni na
nyadhifa muhimu katika baraza la mawaziri na za usalama na ulinzi.
Rais Thein Sein ambaye chama chake cha Union Solidarity and Development
USDP kimeshindwa vibaya na mkuu wa majeshi Min Aung Hlaing wamekipongeza
chama cha NLD kwa ushindi wake na wameahidi kuyaheshimu matokeo ya
uchaguzi huo na kusaidia kuhakikisha kipindi cha mpito cha kukabidhi
madaraka kitaendeshwa kwa amani.
Awali Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alimpongeza Suu Kyi
baada ya chama chake kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu lakini
ameonya bado kuna kazi kubwa mbele ya kujenga demokrasia Myanmar.
Ban ameutaja uchaguzi huo wa kihistoria kama hatua muhimu katika
mchakato wa taifa hilo kuondokana na mfumo wa utawala unaodhibitiwa na
jeshi.
Jumuiya ya kimataifa yampongeza Suu Kyi
Hata hivyo amesikitika kuwa jamii ya walio wachache ya Rohingya
haikuruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo. Ban ameahidi Umoja wa
Mataifa utaisaidia Myanmar ambayo ilikuwa imetengwa kwa muda mrefu na
jumuiya ya kimataifa, kujiimarisha kidemokrasia na kuheshimu haki za
binadamu.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Barack Obama amempigia simu Suu Kyi
kumpongeza na kumsifu kwa juhudi zake za kujitolea kwa miaka mingi
kuendeleza amani na demokrasia Myanmar.
Ban na Obama pia wamempongeza Rais Sein kwa kuandaa kwa ufanisi mkubwa
uchaguzi huo wa kihistoria. Ban amemsifu Sein kwa ujasiri na maono yake
katika uchaguzi huo.
Marekani imesema inatafakari kuiondolea Myanmar baadhi ya vikwazo
ilivyokuwa imeiwekea. Uchaguzi huo wa kwanza kwa chama cha NLD kujitosa
tangu mwaka 1990, umeshuhudia idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza
kukipa ushindi wa zaidi ya asilimia 80.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment