Marekani imefanya mashambulizi ya anga nchini Syria yanayomlenga
''Jihadi John'', raia wa Uingereza anayetuhumiwa kuonekana kwenye video
kadhaa za kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu-IS, zinazoonyesha watu
wakichinjwa.
Mkurugenzi wa habari wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Peter Cook amesema
mashambulizi hayo ya vikosi vya Marekani, yamefanyika usiku wa jana
kwenye ngome muhimu ya IS ya Raqqa, kaskazini mwa Syria.
Amesema mashambulizi hayo yalikuwa yakimlenga Mohammed Emwazi,
anayejulikana pia kama ''Jihadi John'', ambaye amekuwa akionekana kwenye
mikanda ya video inayomuonyesha akiwachinja waandishi wa habari wa
Marekani, Steven Sotloff na James Foley, akiwa kajifunika uso wake.
Raia huyo wa Uingereza pia ameonekana kwenye video za mauaji ya
mfanyakazi wa shirika la misaada la Marekani, Abdul-Rahman Kassig,
wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya Uingereza, David Haines na Alan
Henning, mwandishi wa habari wa Japan, Kenji Goto pamoja na watu wengine
kadhaa waliokuwa wakishikiliwa mateka.
Nalo shirika la kufuatilia haki za binaadamu nchini Syria, lenye
makao yake Uingereza, limesema leo kuwa kiongozi wa IS ambaye ni raia wa
Uingereza na wanamgambo watatu wa kigeni, wameuawa katika mashambulizi
hayo ya Marekani. Hata hivyo shirika hilo, halijaeleza iwapo raia huyo
wa Uingereza ni ''Jihadi John'' au la. Mapema leo Marekani ilisema
huenda Emwazi ameuawa katika mashambulizi hayo.
Cook amesema wanaitathmini operesheni hiyo na watatoa taarifa zaidi kwa
wakati utakaofaa. Vyombo vya habari vya Marekani na Uingereza,
vilimpachika Emwazi jina la ''Jihadi John'', baada ya kundi la watu
walioshikiliwa mateka kusema kwamba alikuwa ni sehemu ya mtandao wa
kigaidi wanaojiita ''The Beatles.''
Mzaliwa wa Kuwait
Emwazi, alizaliwa Kuwait katika familia isiyo na uraia ambayo ina asili
ya Iraq. Wazazi wake walihamia Uingereza mwaka 1993, baada ya juhudi zao
za kupata uraia wa Kuwait, kushindikana.
Mashambulizi hayo ya anga ya Marekani dhidi ya ''Jihadi John''
yamefanyika wakati ambapo vikosi vya Kikurdi vya Peshmerga leo vimeingia
katika mji wa Sinjar, ili kuendesha operesheni ya kuusafisha mji huo wa
kaskazini mwa Iraq, uliokuwa unadhibitiwa na IS.
Vikosi vya Peshmerga vinavyoungwa mkono na mashambulizi ya anga ya
Marekani, jana vilianzisha operesheni waliyoipa jina ''Operesheni ya
kuisafisha Sinjar,'' vilifanikiwa kuifunga barabara kati ya mashariki na
magharibi, wakati vikipambana na wanamgambo wa IS. Kamanda wa Peshmerga
Dyar Namo, anafafanua zaidi.
''Jana baada ya mashambulizi ya anga tukisaidiwa na vikosi vya muungano,
hapakuwa tena na operesheni zao wala mizunguko miongoni mwao. Mji
ulikuwa umetulia,'' alisema Namo.
Taarifa iliyotolewa na baraza la usalama la eneo la Kurdistan katika
mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Twitter, imeeleza kuwa milio
mikubwa ya risasi imesikika ndani ya mji huo, wakati ambapo wapiganaji
hao walijikusanya chini ya mlima wakiuangalia mji huo kutoka upande wa
kaskazini. Watu walioshuhudia wamesema baadhi yao walikuwa wamebeba
mabegani mikanda yenye mabomu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment