Baraza la Usalama linatarajiwa kupiga kura leo kuidhinisha kwa kauli
moja azimio lililotayarishwa na Ufaransa linalolenga kumaliza machafuko
nchini Burundi.
Wengi wanahofia huenda yakaongezeka na kuwa mauaji ya watu wengi kama ilivyotokea nchinji Rwanda.
Azimio hilo la Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
litaanzisha mipango ya Umoja wa Mataifa kuimarisha uwepo wa kimataifa
nchini Burundi pengine kwa kuwapeleka wanajeshi wa kulinda amani baada
ya kushuhudiwa miezi kadhaa ya machafuko.
Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na makundi ya kutetea haki za
binaadamu wameomba kuchukuliwa hatua dhidi ya kile mashahidi wanakiita
kuwa ni ukandamizaji mkubwa wa serikali dhidi ya wapinzani. Kauli
zilizotolewa na maafisa wa serikali wiki iliyopita zikirejelea lugha
iliyotumiwa katika mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994 nchini Rwanda
zimezusha hofu katika Umoja wa Mataifa. Thomas Perriello ni mjumbe
maalum wa Umoja wa Mataifa Kanda ya Maziwa Makuu "Serikali ya Marekani
ina wasiwasi kuhusiana na machafuko na lugha inayotumiwa na serikali ya
Burundi pamoja na ukandamizaji wa vikosi vya usalama na wapinzani wa
serikali. Tuna wasiwasi na matumizi ya nguvu kupita kiasi katika pande
zote na lugha inayohimiza mgawanyiko, iwe ni wa kisiasa au kikabila.
Jamii ya kimataifa inafuatilia kwa makini uchochezi huo".
Wanadiplomasia wa Ufaransa wanasema wanatarajia rasimu ya azimio hilo
kuungwa mkono kwa kauli moja na baraza hilo lenye nchi 15 wanachama.
Ufaransa imesambaza rasimu ya azimio ambalo linatinishia kuwawekea
vikwazo viongozi wa Burundi ambao wanachochea mashambulizi au kuzuia
juhudi za amani.
Azimio hilo litamwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
kuwasilisha mapendekezo kwa baraza hilo katika siku 15 kuhusu hatua
ambazo huenda zikachukuliwa ili kuzuia umwagikaji damu. Maafisa wa Umoja
wa Mataifa wanazungumzia mipango ya kuwapeleka haraka Burundi wanajeshi
wa kulinda amani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - MONUSCO
ikiwa machafuko yatakuwa makubwa kupindukia.
Ujumbe wa MONUSCO nchini Congo una wanajeshi 20,000 pamoja na kikosi
kingine cha dharura kinachowajumuisha wanajeshi maalum kutoka Afrika
Kusini, Malawi na Tanzania ambacho huenda pia kikatumwa Burundi ikiwa
patakuwa na haja. Aidha Umoja wa Afrika umelitaka Jeshi la Dharura la
Afrika Mashariki kuwa tayari wakati kuenda Burundi wakati wowote ikiwa
hali itakuwa mbaya zaidi
Burundi imekumbwa na mauaji, mateso na kuzuiwa watu kinyume cha sheria
tangu Rais Pierre Nkurunziza alitangaza nia yenye utata ya kuurefusha
uongozi wake madarakani mwezi Aprili. Kiasi ya watu 240 wameuawa na
wengine zaidi ya 200,000 wamekimbia nchi hiyo
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment