DEREVA wa basi la Allys Star, Alfa Haji (37) lililokuwa
likitokea katika wilaya ya Kaliua kuelekea jijini Mwanza amefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Urambo mkoani Tabora, akikabiliwa na
mashitaka 22 ikiwemo kusababisha vifo vya watu wanane na majeruhi 13.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Hassani Momba, Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Mkaguzi
Msaidizi, Felibet Pima alisema kwamba Desemba 15 mwaka huu, saa 12:00 asubuhi
katika kijiji cha Vumilia wilaya ya Urambo mtuhumiwa huyo aliendesha gari
kizembe na kusababisha vifo vya watu wanane.
Alisema kwamba licha ya kusababisha vifo vya watu wanane
pia akiendesha gari kwa uzembe alisababisha majeruhi kwa watu 13. Mwendesha
mashitaka huyo aliwataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Hamisi Ramadhani mkazi
wa Magili mkoani Tabora, Grace Andrew (24), ambaye ni mkazi wa Ng’ambo Tabora,
Paschal Abdul (miezi 8) mkazi wa Bunda,Tipwege Kataga (20), Emeliana Tryphon
(24) , Antoni Julius Mkazi wa Wilayani Kaliua, Shija Anton mkazi wa Kaliua na
Rahel Mussa Mkazi wa Ulyankulu wilayani Kaliua.
Aidha Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Pima
aliwataja majeruhi mbele ya Mahakama hiyo kuwa ni Pili Juma (15), Maro Machano
(50), Gift Mayunga (29), Ibrahimu Hasani (25), Rahel Mabula (20) Jane Inosent(
29) Anges Michael na Godlifa Alois (35). Wengine ni Santo Lufasiza (28) Mariamu
Cosmas (38) Fatuma Juma (19) Yunge Sini (9) na Marthar Luhende (21).
Hata hivyo mtuhumiwa huyo alikana mashitaka yote 22 na
amerudishwa rumande baada ya Mahakama kuona ni njia ya kumpatia usalama wake na
kesi hiyo itatajwa tena Desemba 31 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment