SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) limesema tatizo la
kukatika kwa umeme mara kwa mara hasa nyakati za jioni katika maeneo ya
Mbagala, Mtoni Kijichi na Yombo kutokana na mifumo ya umeme katika maeneo hayo
kuzidiwa jambo ambalo wameanza kulishughulikia.
Tayari marekebisho katika mifumo ya umeme ya maeneo hayo
yameanza na inategemewa tatizo hilo kumalizika kuanzia wiki ijayo. Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Felchesmi Mramba wakati
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo pia alisema,
maboresho mengine wanayoyafanya ni pamoja na huduma ya dharura.
Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi
juu ya kuchelewa kushughulikiwa kwa taarifa za hitilafu za umeme na vitengo vya
dharura katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ili kuondoa kero hii shirika limechukua hatua ambazo
zitaanza kutekelezwa kuanzia leo(jana) ambazo ni kuongeza maofisa katika
vitengo hivi ili kushughulikia matatizo haya,” alisema Mramba.
Alisema katika kila ofisi ya dharura kutakuwa na Ofisa wa
huduma kwa wateja na mhandisi ambao watasimamia muda na ubora wa huduma
zinazotolewa kwa wateja wao baada ya kutoa taarifa za dharura.
“Kwa hiyo kuanzia leo (jana) wateja wetu wasije kushangaa
wakapigiwa simu na maofisa wetu na kuwauliza kama taarifa zao zimeshughulikiwa,
watambue hii ni katika maboresho ya vitengo vya dharura,” alisema.
Naye Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Usambazaji Umeme,
Sophia Mgonja alisema, bado wanaendelea na maboresho ya kuhakikisha wateja wao
wanapata huduma nzuri.
0 comments:
Post a Comment