Aliyekuwa meneja wa timu ya taifa ya Uholanzi Guus
Hiddink ameteuliwa kuwa kaimu meneja wa Chelsea hadi mwisho wa msimu.
Ameteuliwa baada ya Jose Mourinho kufutwa Alhamisi.
"Nimefurahia kurejea Stamford Bridge. Chelsea ni
moja ya klabu kubwa duniani lakini haimo pale inakofaa kuwa kwa sasa. Hata
hivyo nina uhakika tunaweza kubadilisha mambo,” amesema Hiddink baada ya
kuteuliwa. “Nasubiri kwa hamu kufanya kazi na wachezaji na wakufunzi wenzangu
wapya katika klabu hii kubwa na kufufua uhusiano wangu mzuri na mashabiki wa
Chelsea.”
Mholanzi huyo alikuwa uwanjani Stamford Bridge kutazama
mechi ya Ligi ya Premia dhidi ya Sunderland ambayo ilisimamiwa na Steve Holland
akisaidiwa na Eddie Newton, ambaye sasa atakuwa kocha msaidizi wa timu.
Hiddink, aliwahi kunoa Chelsea wakati mmoja,
alipowasaidia kushinda Kombe la FA mwaka 2009, lakini bado hajatia saini
mkataba.
The Blues wamo nambari 16 ligini kwa sasa baada ya kushindwa
mechi tisa kati ya 16 walizocheza msimu huu Ligi Kuu Uingereza.
Hiddink alishinda mataji sita ya ligi ya Uholanzi na
Kombe la Ulaya akiwa meneja wa PSV Eindhoven ya Uholanzi katika vipindi viwili.
Pia aliongoza timu za taifa za Korea Kusini, Australia na
Urusi kabla ya kujiunga na Chelsea mara ya kwanza kujaza pengo lililoachwa na
Luiz Felipe Scolari Februari 2009.
Alijiuzulu wadhifa wake kama mkufunzi wa timu ya Taifa ya
Uholanzi mwezi Juni, baada ya kutofanya vyema katika juhudi za kuwasaidia kufuzu
kwa Euro 2016.
Mwishowe Uholanzi hawakufuzu kwa michuano hiyo.
0 comments:
Post a Comment