Viongozi wa zamani wa waasi Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo Thomas Lubanga na Germain Katanga wamepelekwa DR Congo wakakamilishie
vifungo vyao huko.
Wawili hao walifungwa jela na Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu wa Kivita (ICC) baada ya kupatikana na makosa ya uhalifu wa kivita.
Hii ni mara ya kwanza kwa ICC kuwatuma wafungwa nje
wakatumikie vifungo vyao.
Afisi ya Rais wa mahakama ya ICC ilitangaza DR Congo kuwa
taifa litakalotumiwa kutekeleza vifungo vya wawili hao Desemba 8.
Afisi hiyo ilisema Thomas Lubanga Dyilo na Germain
Katanga wenyewe walikuwa wameeleza mapenzi ya kwenda kutumikia vifungo vyao
taifa lao la kuzaliwa.
Mahakama ya ICC itaendelea kufuatilia kufungwa kwao
kuhakikisha wanawekwa katika “mazingira yafaayo kimataifa ya kuwazuilia
wafungwa”.
Wawili hao wamehamishiwa DR Congo kupitia ushirikiano wa
karibu kati ya maafisa wa DR Congo, Uholanzi na Ufaransa.
Lubanga alihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela tarehe 10
Julai, 2012 baada ya kupatikana na makosa ya kuwaandikisha watoto kwenye jeshi
na kuwatumia vitani.
Mahakama ya rufaa ilidumisha hukumu hiyo Desemba 2014.
Lubanga amekuwa kizuizini The Hague tangu 16 Machi 2006 na ukizingatia muda
aliokaa kizuizini kabla ya kuhukumiwa, basi huenda akaachiliwa huru kabla ya
2020.
Katanga alihukumiwa kifungo cha miaka 12 jela kwa maoksa
ya kushiriki kosa la uhalifu dhidi ya binadamu na makosa manne ya uhalifu wa
kivita ya kuua, kushambulia raia na kuharibu mali kijiji cha Bogoro, Ituri
mashariki mwa Dr Congo.
Anatarajiwa kukamilisha kifungo chake tarehe 18 Januari
2016.
0 comments:
Post a Comment