Uganda imesema itaitisha tena mazungumzo ya upatanishi ya
Burundi, kufuatia machafuko yaliyoipeleka nchi hiyo ndogo kwenye kingo za vita
na kuulazimu Umoja wa Afrika kujitayarisha kutuma kikosi cha kuwalinda
raia.
Serikali ya Burundi na pia kundi kubwa zaidi la upinzani
wamekaribisha hatua ya kuanzisha tena mazungumzo hayo. Siku ya Ijumaa,
(18.12.2015) Umoja wa Afrika ulisema unajiandaa kutuma kikosi cha wanajeshi
5,000 nchini Burundi kuwalinda raia, ukitumia nguvu kwa mara ya kwanza kutuma
wanajeshi katika nchi mwanachama dhidi ya matakwa ya nchi hiyo.
Hali ya wasiwasi umekuwa ikiongezeka nchini Burundi hasa
tangu watu wenye silaha walipovamia kambi za kijeshi katika mji mkuu Bujumbura
wiki iliyopita, na kuzusha hofu katika kanda hiyo ambako kumbukumbu za mauaji
ya kimbari ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda zingalipo.
Burundi ilitumbukia katika mgogoro mwezi Aprili baada ya
Rais Pierre Nkurunziza kutangaza mipango ya kuwania muhula wa tatu madarakani.
Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 400 wameuawa tangu mwezi Aprili,
wakati uamuzi huo wa Nkurunziza ulipozusha maandamano na baadae jaribio la
mapinduzi lililoshindwa.
Serikali yasema iko tayari
Waziri wa ulinzi wa Uganda Chrispus Kiyonga, aliuambia
mkutano wa wandishi wa habari mjini Kampala siku ya Jumamosi, kwamba hali ya
usalama nchini Burundi imekuwa ikidorora kila kukicha. "Tunadhani sasa ni
wakati muafaka na muhimu kuanzisha tena majadiliano," alisema Kiyonga.
Kiyonga alisema karibu makundi 14 yanayowakilisha
matabaka mbalimbali ya jamii ya Burundi, kikiwemo chama tawala, vyama vya
upinzani na mashirika ya kiraia yatahudhuria mazungumzo hayo.
Msemaji wa serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba
alisema serikali imekuwa tayari wakati wote kufanya mazungumzo na ilikuwa
inasubiri mwaliko. "Ni mazungumzo ya Warundi na ni Warundi tu watakaoamua
nini cha kujadiliana," aliliambia shirika la habari la Reuters.
Nzobonariba hata hivyo aliondoa uwezekano wa kuzungumza
na yeyote ambaye serikali inamchukulia kuwa mhusika katika jaribio la mapinduzi
lililofeli. "Linaweza kuwa tukio la kutuwezesha kuwakamata kwa sababu
wanatafutwa na vyombo vya sheria vya Burundi," alisema.
Mazungumzo kuanza Desemba 28
Pancrace Cimpaye, msemaji wa muungano mkubwa zaidi wa
upinzani nchini Burundi unaojulikana kama CNARED, alikaribisha hatua ya Uganda
kuitisha upya mazungumzo ya amani, inagwa alisema mungano wake ulikuwa bado
haujapatiwa mwaliko.
"Kwetu mazungumzo ni kati ya pande mbili kwenye
mgogoro, na pande hizo mbili zinazozozana ni Nkurunziza na serikali yake kwa
upande mmoja, na CNARED kwa upande mwingine," aliliambia shirika la
Reuters.
Mazungumzo hayo yataanza tena nchini Uganda Desemba 28,
na baadae yatahamishiwa mjini Arusha nchini Tanzania, yaliko makao makuu ya
jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo Burundi ni mwanachama wake.
Mwezi Julai jumuiya ya Afrika Mashariki ilimeteua Rais wa
Uganda Yoweri Kaguta Museveni kuwa mpatanishi wa mgogoro huo na mikutano ya
awali ilifanyika katika mji mkuu wa Burundi katika mwezi huo.
Hali yazidi kuwa mbaya
Katika mapigano mabaya zaidi tangu jaribio la mapinduzi
lililoshindwa mwezi Mei, waasi walizishambulia kambi za kijeshi katika mji mkuu
wa Burundi; Bujumbura wiki iliyopita, ambapo karibu watu 90 waliuawa.
Mashirika ya kuteteta haki za binaadamu yameripoti kuwepo
na makabiliano mabaya kati ya waandamanaji na vikosi vya serikali, mashambulizi
ya silaha na kuwekwa vizuwizini wakosoaji wa serikali. Lakini serikali imepuuza
ripoti za ukiukaji wa haki za binaadamu.
Mamia ya maelfu ya Warundi wameikimbia nchi hiyo kunusuru
maisha yao tangu ulipoibuka mgogoro huo mbaya zaidi kuikumba Burundi tangu
ilipotoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa na mwelekeo wa
kikabila mwaka 2005.
0 comments:
Post a Comment