Image
Image

Majaliwa afanya ukaguzi ujenzi wa mradi wa mabasi ya (DARTS)*Asema january 10 yanaanza kazi.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) na wadau wote kuhakikisha kuwa mradi huo unaanza kufanya kazi ifikapo Januari 10, 2016 kama walivyokubaliana kwenye kikao cha Novemba 27, 2015.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Desemba 19, 2015) wakati akizungumza na viongozi wa TAMISEMI, TANROADS, watendaji wa mradi huo, viongozi wa mkoa na Manispaa ya Kinondoni mara baada ya kumaliza kukagua mradi huo katika eneo la Morroco, jijini Dar es Salaam.
“Nataka kusisitiza kuwa ahadi ya kuanza kutoa tarehe 10 Januari 2016 iko palepale. Fanyeni mapitio na mwendeshaji wenu mjiridhishe juu ya vipengele vyote vya mkataba. Badilisheni tiles za pale Feri kwa sababu mlishaambiwa kwamba ziko chini ya kiwango na mkakubali,” alisema.
Kuhusu moshi unaotoka kwenye soko la samaki la Feri, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam wasimamie suala hilo kwa sababu Manispaa ya Ilala (ambao wanasimamia soko hilo) wako chini yao. “Mlisema mtabadilisha mfumo wa majiko lakini naona hakuna kilichofanyika. Nitakapokuja kukagua tena mradi huu mwisho wa mwezi, nitapita Feri kuona kama mmetekeleza agizo hilo,” aliongeza.
“Na hapa hamna jinsi, ama mbadilishe mfumo wenu wa majiko muweke yasiyotumia kuni na kutoa moshi kiasi kile au mtafute mahali pengine pa kuhamishia hilo soko ili watu waendelee na biashara zao,” alisema.
Amewataka wanasheria wa ofisi zote zinahusika na mradi huo wahakikishe kuwa wanasimamia mikataba na kuipitia upya ili wamiliki wa daladala ambao ni wadau wakuu wa mradi huo nao pia wasiachwe wakati mradi unaanza.
“Mwendeshaji wa UDART ambaye anaungana na waendeshaji wa daladala hakikisheni wanaingia kwenye mpango huo bila malalamiko. Wenye daladala ni watu ambao tumewatoa kwenye route zao, simamieni mikataba hii ili kusiwe na malalamiko yoyote  juu ya umiliki,” alisema.
Alisema watoa huduma za uendeshaji ni lazima wafanye kazi sambamba na Serikali kwani ndiye mdau mkuu. DART ni wakala wa Serikali  lakini UDART (UDA Rapid Transport) ni kampuni ya binafsi  inayotoa huduma za mpito katika miundombinu ya DART. Huduma hizo ni pamoja na mabasi yanayotoa huduma, ukataji wa tiketi na huduma za ujazaji salio kwenye tiketi hizo.
UDART inamilikiwa kwa pamoja na shirika la UDA pamoja na muunganiko wa wamiliki wa Daladala ambao hadi sasa kuna DARCOBOA na UWADAR.
Waziri Mkuu alifanya ukaguzi wa miundombinu ya DART Kuanzia Feri hadi Kimara na kurudi kisha akaanzia Magomeni hadi Morocco. Pia alikagua depot ya mabasi ya mradi iliyopo Jangwani na kuridhika na hatua ambazo zimechukuliwa hadi sasa. Alikuwa akifuatilia utekelezaji wa maagizo aliyowapa Novemba 27, mwaka huu kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake. Ameahidi kurudi na kukagua tena mradi huo mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akitembelea maeneo mbalimbali ya kituo cha Feri jijini Dar es Salaam leo.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akipanda basi la mwendo wa haraka mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali katika kituo cha feri leo jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kumalizia kukagua ujenzi wa barabara ya mradi wa mabasi yaendayo haraka katika kituo cha Morocco jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na watendaqji mbalimbali wa mradi wa mabasi yaendayo haraka waliofika katika kituo cha Feri cha Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) leo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika kituo cha Mradi wa mabasi cha Jangwani kukagua maendeleo ya ujenzi ya kituo hicho ikiwa ujenzi wa kituo hicho upo hatua za mwisho kukamilika.
 Kituo cha Mradi wa mabasi yaendayo haraka kikiwa kimekamilika na mabasi yakiwa nyuma ya kituo hiki kwaajili yakisubiri kumalizika kwa barabara ili ifikapo Januari 10, 2016 kuanza kufanya kazi.
Mabasi ya mwendo wa haraka yakiwa kwenye maegesho.  
Picha na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment